Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kongamano maalumu DSM lasailia matumizi ya Kiswahili fasaha katika vyombo vya habari

Kongamano maalumu DSM lasailia matumizi ya Kiswahili fasaha katika vyombo vya habari

Hivi karibuni mjini Dar es Salaam, Tanzania kulifanyika Mkutano wa Kimataifa wa Idhaa za Kiswahili ambapo kulisailiwa taratibu za kuchukuliwa kipamoja kueneza matumizi sahihi, sanifu na fasaha ya lugha ili kujenga mazingira mapya ya utangazaji. Kongamano hili liliandaliwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA)na kuhudhuriwa na mashirika kadha ya redio na televisheni, ikiwemo pia Idhaa ya Redio ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa wa BAKITA, Suleiman Hegga, moja ya maazimio yaliopitishwa ni lile pendekezo linalotilia mkazo umuhimu wa kupunguza makosa ya utumiaji wa Kiswahili kisicho sahihi katika utangazaji, tatizo liliochipuka katika kipindi cha karibuni baada ya kukithiri kwa wadau wa lugha ya Kiswahili, ndani na nje ya Afrika ya Mashariki. Kwenye kipindi, tumeandaa mahojiano na Mwenyekiti Hegga ambaye anafafanua umuhimu wa idhaa zinazotumia Kiswahili kuimarisha matumizi ya Kiswahili sanifu.

Nilihudhuria mkutano wa BAKITA kwa niaba ya Idara ya Habari ya UM (DPI) na Idhaa ya Redio ya Umoja wa Mataifa, na nilichukua fursa hiyo kumhoji pia Profesa Jumanne Mayoka, wa Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro, Tanzania. Kwenye mazungumzo hayo Profesa Mayoka anatuchambulia natija alizoashiria zitapatikana, baada ya mkutano kumaliza mijadala yake, katika kukuza na kuendeleza matumizi bora ya Kiswahili kwenye vyombo vya habari vya kitaifa na kimataifa.

Sikiliza maelezo kamili kwenye idhaa ya mtandao.