Skip to main content

Jamii ya Shompole kupokea Zawadi ya Ikweta

Jamii ya Shompole kupokea Zawadi ya Ikweta

Mnamo mwezi Januari 2002, Shirika la UM juu ya Miradi ya Maendeleo (UNDP) lilianzisha mpango maalumu uloikuwa na madhumuni ya kudumisha utunzaji wa viumbe anuwai na kuimarisha hifadhi ya mazingira, hasa kwenye zile sehemu za joto za tropiki.

Washindi watano walifanikiwa kupokea Tunzo ya Ikweta kwa mwaka 2006, kati ya washindani wa fainali 25 ambao walichaguliwa kutoka wateuliwa 300. Washindi wa Tunzo ya Ikweta kwa 2006 walitokea Bukini, Kenya, Guatemala, Kisiwa cha Isabele, Ecuador pamoja na Bangladesh. Kenya na Bukini waliwakilisha washindi wa Bara la Afrika. Kijiji cha Andavadoaka, Bukini kilishinda Tunzo ya Ikweta kwa sababu ya kufanikiwa kuboresha uvuvi wa pweza na kwa kuhakikisha kuwa mali hii ya asili itadumu. Halkadhalika, Jamii ya Wamaasai ya Shompole kutoka Kenya ilibarikiwa Tunzo ya Ikweta kwa kufanikiwa kutunza kanda za eneo kubwa za mbuga zenye mandhari nzuri, ambazo zilitumiwa kuendeleza aina ya utalii uliohifadhi mazingira, shughuli ambazo vile vile ziliwapatia wenyeji wa KiMaasai natija za kiuchumi.

Ole Petenya Yusuf-Shani, anayewakilisha jamii ya Shompole alizuru Makao Makuu ya UM kupokea Tunzo ya Ikweta, na alikuwa na mazungumzo na Redio ya UM ambapo alelezea juu ya historia ya shirika lao na kazi wanazozihudumia kuboresha maisha kijumla.

Sikiliza mazungumzo kamili kwenye idhaa ya mtandao.