Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Usomali kuwalazimisha maelfu ya raia kuhajiri Yemen kutafuta hifadhi

Mapigano Usomali kuwalazimisha maelfu ya raia kuhajiri Yemen kutafuta hifadhi

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) kwenye taarifa iliyoiwasilisha Geneva, Ijumanne asubuhi, ilieleza mapigano yenye kuendelea hivi sasa kwenye mji wa Mogadishu, na katika eneo la kati la Usomali, yamesababisha maelfu ya raia kuhatarisha maisha kwa kuhama makwao, na kuamua kufanya safari hatari ya kuvuka Ghuba ya Aden, kuelekea Yemen kuomba hifadhi.

Kwa mujibu wa traarifa zilizopokewa na UNHCR kutokea mtandao wa washiriki wenzi waliopo Usomali, inakadiriwa ya kuwa tangu tarehe 7 Mei mwaka huu, watu 12,000 walihajiri makwao na kuelekea mji wa Bossaso, uliopo kaskazini ya Usomali ili kupata makazi ya muda, wakati wakisubiri fursa ya kuihama nchi, pindi watapata wafanya magendo walio tayari kuwavusha kwenye Ghuba ya Aden katika mashua zisio madhubuti. Wahamiaji hawa wa ndani ya nchi (IDPs) ni miongoni mwa Wasomali 232,000 waliolazimika kuhajiri mastakimu yao baada ya mapigano kuripuka kwenye wilaya kadha za nchi, na vile vile katika mji mkuu wa Mogadishu, mnamo mwanzo wa mwezi Mei, baina ya majeshi ya mgambo ya upinzani ya Al-Shabaab na Hizb-al-Islam dhidi ya vikosi vya Serikali. UNHCR inasisitiza mradi wenye uwezo wa kukomesha magendo ya kutorosha raia wa Usomali wanaopelekwa Yemen, kwa kupitia eneo hatari la Ghuba ya Aden, ni ule utakaoleta suluhu ya kisiasa juu ya mgogoro wa Usomali.