Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Joto linazidi kupanda duniani ni changamoto ambayo lazima tukabiliane nayo sasa: UN

Halijoto imefikia rekodi ya juu kote ulimwenguni mwaka 2024.
© Unsplash/Timo Volz
Halijoto imefikia rekodi ya juu kote ulimwenguni mwaka 2024.

Joto linazidi kupanda duniani ni changamoto ambayo lazima tukabiliane nayo sasa: UN

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo ametoa wito wa dharura wa kuchukua hatua ili kulinda vyema mabilioni ya watu duniani kote walioathiriwa na athari za joto kali, huku ongezeko la joto duniani likiendelea kupanda bila dalili ya kupungua.

Wito huo umekuja wakati hali ya joto kali na mawimbi mabaya ya joto kuanzia Marekani hadi Ukanda wa Sahel Afrika na Ulaya hadi Mashariki ya Kati ambayo yameua mamia ya watu msimu huu wa joto.

Taarifa yake inasema wakati wa Hija kwa mfano, joto kali liligharimu maisha ya zaidi ya mahujaji 1,300.

António Guterres amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York akiongeza kuwa "Mabilioni ya watu wanakabiliwa na janga la joto kali linaghubikwa na mawimbi ya joto yanayozidi kukatili maisha huku halijoto ikizidi nyuzi joto 50 kote ulimwenguni. Hiyo ni nyuzi joto 122 Fahrenheit ikiwa ni nusu ya kiwango cha kuchemka,”

Ameendelea kusema kwamba "Ujumbe uko bayana, joto linapanda. Joto kali lina athari kubwa kwa watu na sayari. Ulimwengu lazima ukabiliane na changamoto ya kupanda kwa halijoto.”

Mfanyakazi wa nyumbani anafagia barabara katika mtaa wa moja huko Delhi, India.
© ILO/Marcel Crozet
Mfanyakazi wa nyumbani anafagia barabara katika mtaa wa moja huko Delhi, India.

Kuwalinda walio hatarini zaidi

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba ingawa "joto lenye athari mbaya liko kila mahali haliathiri kila mtu kwa usawa”.

Wale walio katika hatari zaidi ni pamoja na maskini wa mijini, wanawake wajawazito, watoto, wazee, wale wenye ulemavu, wagonjwa, na waliokimbia makazi yao, ambao mara nyingi wanaishi katika makazi duni bila kupata viyoyozi.

Kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa, vifo vinavyotokana na joto kwa watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 viliongezeka kwa takriban asilimia 85 katika miongo miwili iliyopita, wakati asilimia 25 ya watoto wote hivi leo wanakabiliwa na joto la mara kwa mara na ifikapo 2050, idadi ianaweza kuongezeka hadi karibu asilimia 100.

"Lazima tuchukue hatua kwa kuongeza kwa kiasi kikubwamifumo ya kupooza inayotoa kiasi kidogo cha hewa ukaa, kwa mfano kwa kutumia suluhu za asili, mipango miji na kusafisha teknolojia za kupoeza huku tukiimarisha ufanisi wake," amesema Guterres, akitoa wito wa kuongeza fedha ili kulinda jamii dhidi ya janga la tabianchi.

Wafanyakazi wa ujenzi wakitembea kando ya barabara huko Daan Hari, Ufilipino.
© ILO/Bobot Go
Wafanyakazi wa ujenzi wakitembea kando ya barabara huko Daan Hari, Ufilipino.

Kulinda wafanyakazi

Bwana Guterres pia alisisitiza haja ya kuimarisha ulinzi kwa wafanyakazi.

Zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi duniani, au watu bilioni 2.4, wako katika hatari kubwa ya joto kali, kulingana na ripoti mpya ya Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa ILO.

ILO inasema hali ni mbaya hasa katika kanda za Afrika ambako  zaidi ya asilimia 90 na nchi za Kiarabu,  zaidi ya asilimia 80 ya wafanyakazi wako katika hatarimya joto hilo.

Katika nchi za Asia na Pasifiki eneo lenye watu wengi zaidi ulimwenguni idadi ya wafanyakazi walio hatarini ni watu watatu kati ya wafanyikazi wanne  ambayo ni asilimia 75.

Kwa kuongezea, Katibu Mkuu Guterres amesema msongo wa joto kazini unakadiriwa kugharimu uchumi wa dunia dola trilioni 2.4 ifikapo mwaka 2030, kutoka dola bilioni 280 katikati ya miaka ya 1990.

"Tunahitaji hatua za kulinda wafanyakazi, kwa kuzingatia haki za binadamu," amesisitiza Bwana Guterres na kuongeza kuwa "ni lazima tuhakikishe kwamba sheria na kanuni zinaonyesha ukweli wa joto kali hivi sasa na zinatekelezwa."

Kuimarisha mnepo

Guterres pia amesisitiza haja ya kuimarisha mnepo wa uchumi na jamii, akitaja athari kama vile uharibifu wa miundombinu, kuharibika kwa mazao, na kuongezeka kwa shinikizo kwenye usambazaji wa maji, mifumo ya afya, na gridi za umeme.

Miji iko hatarini zaidi, inapata joto mara mbili ya kiwango cha wastani cha kimataifa.

Ili kukabiliana na changamoto hizi, Bwana. Guterres ametoa wito wa kuwepo kwa mipango ya utekelezaji ya kina na iliyolengwa kulingana na takwimu za kisayansi ni muhimu kwa nchi, miji na sekta.

"Tunahitaji juhudi za pamoja ili kuwa na uchumi usio na joto, sekta muhimu, na mazingira yaliyojengwa vyema."

Viwango vya juu vya halijoto vinaathiri wafanyikazi wa kilimo huko Jalisco, Meksiko.
© ILO/Rafael Duarte
Viwango vya juu vya halijoto vinaathiri wafanyikazi wa kilimo huko Jalisco, Meksiko.

Kupambana na janga hili

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amerejea kusisitiza kuwa ni muhimu kutambua dalili nyingi zaidi zinazochangia  joto kali, kama vile vimbunga, mafuriko, ukame, moto wa nyika na kupanda kwa kina cha bahari.

Suala la msingi ni kujenga mnepo kuachana na utegemezi wa nishati ya mafuta kisukuku na kutochukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi amesema, Guterres akisisitiza kwamba serikali, haswa mataifa ya G20, sekta kibinafsi, miji na kanda, lazima zipitishe haraka mipango ya hatua  dhidi ya mmabadiliko ya tabianchi ili kupunguza ongezeko la joto duniani hadi kusalia katika nyuzi joto 1.5 ° C.

Kando na hayo, nchi lazima ziondoe mafuta kisukuku kwa haraka na kuachana na miradi mipya ya makaa ya mawe.

"Lazima wafanye kana kwamba mustakabali wetu unategemea hilo kwa sababu ndivyo ilivyo."