Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea Sudan: Ujumbe wa UN wa kutafuta ukweli

Mariam Djimé Adam, mwenye umri wa miaka 33 mkimbizi kutoka Sudan akiwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Adre nchini Chad ambayo sasa inatumika kuhifadhi wakimbizi
© UNICEF/Mahamat
Mariam Djimé Adam, mwenye umri wa miaka 33 mkimbizi kutoka Sudan akiwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Adre nchini Chad ambayo sasa inatumika kuhifadhi wakimbizi

Ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaendelea Sudan: Ujumbe wa UN wa kutafuta ukweli

Amani na Usalama

Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa  wa kutafuta ukweli nchini Sudan umetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza haraka juhudi za kumaliza vita vya nchi hiyo, ukisema umeorodhesha mwenendo wa kutatanisha wa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wakati wa ziara yake ya wiki tatu kwenye nchi jirani ya Chad.

Ujumbe huo wa kutafuta ukweli ulitembelea Chad kuanzia tarehe 30 Juni hadi 18 Julai. Ukiwa huko ulikutana na waathirika na manusura wa mzozo unaoendelea  nchini Sudan pamoja na wanachama wa jumuiya ya kiraia ya Sudan, jumuiya ya wanadiplomasia na timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo.

Ujumbe huo ulisafiri hadi mashariki mwa Chad, ukijumuisha maeneo ya Adre, Farchana na Abeche.

Wakati ujumbe unatambua juhudi kubwa zilizofanywa na mamlaka ya Chad na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na watoa huduma wengine wa mstari wa mbele wa kibinadamu, ni wazi kwamba mahitaji yanazidi msaada unaopatikana.

Mohamed Chande Othman, Mwenyekiti wa Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli amesema "Mgogoro huu unahitaji kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla. Vyombo vya Umoja wa Mataifa na vikundi vya kibinadamu vinahitaji sana msaada wa kifedha na mwingine ili kuhakikisha wakimbizi wa Sudan na waliorejea Chad wanapata huduma za msingi, ikiwa ni pamoja na lishe, mahitaji ya usafi, huduma za afya, na elimu."

Jumuisha ya kimataifa iongeze msaada

Ujumbe huo pia umetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wa kibinadamu kwa jumuiya za Chad zinazohifadhi wakimbizi, ikitaja shinikizo kubwa walilonalo.

Mji wa mpakani wa Chad wa Adre pekee unahifadhi zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Sudan, ikiwa ni mara tano ya uwezo wake.

Jumuiya ya wakimbizi ambayo Ujumnbe huo ilikutana nayo ilielezea ghasia walizokumbana nazo kibinafsi zilizowafanya kutoroka Sudan.

Wameeleza kwa kina matukio ya kutisha ya mauaji, ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ubakaji wa magenge, kuwekwa kizuizini kiholela, utesaji, kutoweshwa, uporaji, uchomaji wa nyumba na matumizi ya askari watoto.

Ukiukaji mwingi unaonekana kulengwa hasa dhidi ya wataalamu kama vile wanasheria, watetezi wa haki za binadamu, walimu na madaktari na watu kufuruhwa makwao imekuwa kitu cha kawaida

"Ninashangaa ujasiri wa wajane wengi ambao tumekutana nao katika kambi," amesema mmoja wa wajumbe hao Joy Ngozi Ezeilo akiongeza kuwa "Hakuna mtu anayestahili kupitia uzoefu wa kikatili wa kubadilisha maisha. Mbali na kupoteza waume na wapenzi wao, wanawake hao wanajitwika peke yao jukumu la kulisha, kusomesha na kulea watoto wao wengi, huku wakipoteza nyumba zao na njia za kujikimu. Wanahitaji kuungwa mkono katika ngazi zote.”

Nini kifanyike

Ujumbe huo wa Kutafuta Ukweli pia umesikia maoni juu ya hatua zinazoweza na zinapaswa kuchukuliwa ili kuvunja mzunguko wa mara kwa mara wa vurugu, na kuhakikisha uwajibikaji kwa wale waliohusika katika ukatili, pamoja na haki na msaada kwa waathirika.

"Hali ilikuwa ya kukatisha tamaa kusikia shuhuda za waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia," amesema mjumbe mwingine Mona Rishmawi.

Ameongeza kuwa "Vurugu hizi zinaonekana kutokea wakati wa utumwa na wakati wanawake na wasichana wanakimbia. Wakati mwingine ni kuadhibu mwanamke ambaye anasimama kikamilifu kwa jamii yake. Wakati mwingine ni bahatinasibu na fursa. Vitendo hivi vya kinyama vikome na wahusika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Waathiriwa pia wanahitaji msaada mkubwa wa kimwili na kisaikolojia, ambao haupatikani kwao sasa.”

Mapigano kati ya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka yameua maelfu ya watu tangu yalipoanza katikati ya mwezi Aprili mwaka jana.

Zaidi ya watu milioni 26 wanahitaji msaada haraka na hawana uhakika wa chakula. Zaidi ya raia milioni kumi wamekimbia makazi yao ndaniya nchi , na zaidi ya wakimbizi milioni mbili wameikimbia nchi, kulingana na Umoja wa Mataifa huku watu zaidi ya 600,000 kati yao waliishia Chad.