Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la joto liliendelea hadi mwezi juni - WMO

Halijoto imefikia rekodi ya juu kuwahi tokea kote ulimwenguni mnamo 2023.
© Unsplash/Ryan Loughlin
Halijoto imefikia rekodi ya juu kuwahi tokea kote ulimwenguni mnamo 2023.

Ongezeko la joto liliendelea hadi mwezi juni - WMO

Tabianchi na mazingira

Kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Huduma ya Mabadiliko ya Tabia nchi ya Muungano wa Ulaya ya Copernicus, wastani wa hali joto duniani umekuwa juu ya nyuzi joto 1.5 za Selsiasi kwa miezi 12 mfululizo jambo ambalo si la kawaida na mara ya mwisho kushuhudia hali kama hii ilikuwa mwaka 2015/2018.

Data za Huduma ya Mabadiliko ya Tabia nchi ya Muungano wa Ulaya, Copernicus ERA5, zinaonesha kwamba mwezi juni ulikuwa na nyuzi joto 1.50 za Selsiasi juu ya makadirio ya awali ya Mwezi Juni kwa mwaka 1850 – 1900 wakati wa mapinduzi ya viwanda ikiwa huu ni mwezi wa 12 mfululizo hali joto kuvuka nyuzi joto 1.5.

“Takwimu hizi za hivi karibuni  kutoka kwa Huduma ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa ya Copernicus kwa bahati mbaya zinaangazia kwamba tutakuwa tukizidi kiwango cha nyuzijoto 1.5 za selsiasi kwa muda na kuongezeka kwa marudio, kila mwezi. Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kwamba ukiukaji wa muda mfupi haumaanishi kuwa lengo la 1.5 °C litapotea kabisa kwa sababu hii inahusu ongezeko la joto la muda mrefu kwa angalau miongo miwili," Anasema Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Celeste Saulo.

Katika mkataba wa Paris, nchi zilikubaliana kuweka wastani wa halijoto wa muda mrefu  kuwa ni chini ya nyuzi joto 2 kabla ya kuanza kwa viwanda na baadae wakaweka kikomo hadi nyuzi joto 1.5 kufikia mwisho wa karne hii, huku wanasayansi wameonya mara kwa mara kwamba ongezeko la joto la zaidi ya nyuzi joto 1.5 linasababisha athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi.

Hata, Katika viwango vya sasa vya ongezeko la joto duniani, tayari kuna athari mbaya za hali ya hewa ambazo ni Pamoja na joto kali, mvua kali na ukame, barafu ya bahari, kuongeza kasi ya kupanda kwa kina cha bahari na joto la bahari.

"Juni ilishuhudiwa kuenea na kuongezeka kwa joto kwa muda mrefu katika nchi nyingi, na athari kubwa katika nyanja zote za maisha ya watu. Hii ilikuwa hata kabla ya kilele cha jadi cha majira ya joto ya kaskazini mwa ulimwengu, ambayo bila shaka itaona joto kali zaidi. Halijoto iliyorekodiwa kwenye uso wa bahari inatia wasiwasi mkubwa kwa mifumo ya ikolojia ya baharini na pia inatoa nishati kwa vimbunga vya kitropiki vinavyoshangaza zaidi - kama tulivyoona kwenye Kimbunga Beryl," Amesema Celeste Saulo.

WMO hutumia hifadhi data sita za kimataifa, ikiwa ni pamoja na ERA5, kwa hali yake ya ufuatiliaji wa tabianchi. Ni muhimu kutambua kwamba hifadhi data nyingine huenda zisithibitishe mfululizo wa miezi 12 ulioangaziwa na Huduma ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Copernicus, kutokana na ukingo mdogo zaidi ya nyuzi joto 1.5 ya viwango vya joto duniani ERA5 kwa Julai na Agosti 2023 na Mei na Juni 2024.

Mkurugenzi wa Huduma ya Mabadiliko ya Tabianchi ya Copernicus, Carlo Buontempo anatoa tahadhari kwamba hata kama hali hii ya kuongeza kwa hali joto itaisha kwa wakati Fulani, lakini kuna uwezekano mkubwa wa jambo hili kujirudia tena, hivyo dunia inapaswa kuangalia namna ya kuacha kuongeza hewa chafu kwenye ang ana bahari ili kuepukana na athari za baadae endapo jambo hili litajirudia tena.