Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC dhuluma nyingi dhidi ya watoto Kivu Kaskazini zinafanyika maeneo ya mapigano: UNHCR

Watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara nyingi hukumbwa na mashambulizi ya kiholela huku mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
UNHCR/S. Modola
Watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara nyingi hukumbwa na mashambulizi ya kiholela huku mapigano yakiendelea kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.

DRC dhuluma nyingi dhidi ya watoto Kivu Kaskazini zinafanyika maeneo ya mapigano: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Mbali na mauaji, watoto wamekuwa ni waathirika wakubwa wa utekaji nyara, unyanyasaji wa kingono, lakini pia kuandikishwa na kutumiwa na makundi yenye silaha vitani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR likibainisha kuwa dhuluma nyingi dhidi ya watoto hao Kivu Kaskazini hutokea katika maeneo ya mapigano.

Kulingana na UNHCR, kesi 164 za ukiukwaji wa haki za watoto ziliripotiwa mwezi wa Mei, ambapo zaidi ya nusu zikiwa ni kesi 91 zilikuwa ni za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Ripoti hiyo ya hali ya watoto ya UNHCR inabainisha kesi za mauaji na ukeketaji wa watoto kuwa ni asilimia 36, vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa dhidi ya watoto ni asilimia 25, kuandikishwa na kutumia watoto vitani asilimia 18, na utekaji nyara wa watoto ni asilimia 19.

Vitendo vingi vya ukiukaji huu mkubwa kwa asilimia 87 ulirekodiwa katika maeneo ya mapigano, wakati wa uondoaji wa wahusika waliohusika katika vita au katika maeneo yanayodhibitiwa na vikundi vyenye silaha. 

"Maeneo haya yameshuhudia ongezeko la mauaji ya watoto kwa mabomu na unyanyasaji wa kijinsia na kuajiriwa jeshini, hasa katika eneo la Nyiragongo," ameeleza kwa kina Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Filippo Grandi katika ripoti yake.

MONUSCO na wadau wamefanikisha kuachiwa huru kwa watoto 12 waliokuwa wanashikiliwa na kikundi kilichojihami cha UFDPC huko Kivu Kaskazini nchini DRC kupitia mpango wa PDDRCS.
MONUSCO
MONUSCO na wadau wamefanikisha kuachiwa huru kwa watoto 12 waliokuwa wanashikiliwa na kikundi kilichojihami cha UFDPC huko Kivu Kaskazini nchini DRC kupitia mpango wa PDDRCS.

Vitendo 1,000 vya ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto mashariki mwa DRC

Kwa kina taarifa hiyo ya UNHCR inaonyesha kwamba huko Beni, watoto walidaiwa kutekwa nyara na kundi la Allied Democratic Forces ADF wakati wa mashambulizi mbalimbali. 

Huko Nyiragongo, kuandikishwa na kutumiwa kwa baadhi ya watoto katika kundi lenye silaha kulibainishwa.

“Eneo la Rutshuru, vikundi vya Mutanda, Bishusha, Bambu, Kihondo na Kanyabayonga viliathirika na mauaji na ukeketaji wa watoto, utekaji nyara na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa dhidi ya watoto katika mazingira ya mapigano na kulipiza kisasi.”

Shirika hilo la wakimbizi limekumbusha kuwa Umoja wa Mataifa ulithibitisha zaidi ya vitendo 1000 vya ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto katika majimbo matatu ya Mashariki mwa DRC ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini katika robo ya kwanza ya mwaka huu. 

Hili linawakilisha ongezeko la 30% kutoka robo ya mwisho ya 2023, na uajiri na utumiaji wa watoto vitani ukiwa umeenea zaidi. 

Mwezi Aprili 2024 pekee, zaidi ya vitendo 450 vya ukiukwaji dhidi ya watoto vilithibitishwa kote mashariki mwa nchi hiyo.

Zaidi ya hayo, unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto uliendelea kuwa juu mwaka 2023 na kuongezeka zaidi mwaka 2024. 

Mwezi Mei, kesi 150 za ukatili wa kijinsia GBV, zilirekodiwa, ambapo zaidi ya robo tatu ambazo ni kesi 114 zilikuwa za ubakaji.

Baba wa watoto sita anatafuta usalama kwa familia yake katika eneo la makazi ya muda karibu na Goma baada ya mkewe kuuawa na bomu huko Sake, jimbo la Kivu Kaskazini. (Maktaba)
© UNHCR/Blaise Sanyila
Baba wa watoto sita anatafuta usalama kwa familia yake katika eneo la makazi ya muda karibu na Goma baada ya mkewe kuuawa na bomu huko Sake, jimbo la Kivu Kaskazini. (Maktaba)

Mapigano kati ya M23 na jeshi la Congo

Kwa mujibu wa UNHCR kwa kiasi kikubwa ubakaji huu 97% ulifanyika katika maeneo yaliyoondolewa wanamgambo wenye silaha na mapigano huko Masisi, Rutshuru, na vile vile katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi wa ndani huko Goma na Nyiragongo. 

Kesi mbayá zaidi za GBV zilibainika haswa katika maeneo ya Mweso, Nyiragongo, Kirotshe, Kibirizi na Katoyi.

Kwa upana zaidi, tathimini ya ulinzi imeorodhesha zaidi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu 1,400 katika jimbo la Kivu Kaskazini. 

Watu waliorejea na waliokimbia makazi yao ambao ni wakimbizi wa ndani wanasalia kuathirika zaidi na ukiukaji huu. 

Kwa mujibu wa tathimini maeneo yaliyoathirika zaidi ni Masisi, Beni na Rutshuru.

Umoja wa Mataifa, unasema hili ni ongezeko la karibu 5% ya ukiukaji na unyanyasaji tangu mwezi Aprili. 

Ongezeko hili linaweza kuhusishwa na kuendelea kwa mapigano kati ya kundi la M23, vikundi vingine vyenye silaha na vikosi vya wanajeshi vya DRC (FARDC) katika maeneo ya kusini mashariki mwa Masisi na kaskazini mwa Rutshuru. Mapigano haya yalisababisha watu wengi kuhama makazi yao, haswa kuelekea kusini mwa Lubero.

Matukio haya ya hivi karibuni yanakuja huku kukiwa na kuendelea kwa mapigano mashariki mwa DRC, hasa mapigano kati ya M23, makundi mengine yenye silaha na FARDC. 

"Mapigano haya yalikaribia mji wa Kanyabayonga na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao na ukiukwaji wa haki za binadamu," limehitimisha shirika la UNHCR.