Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muongo uliopita ndio ulikuwa na joto la kupindukia katika historia: WMO Ripoti

Kuongezeka kwa matumizi ya mafuta ya kisukuku hakuendani na kupunguza ongezeko la joto duniani.
© Unsplash/Johannes Plenio
Kuongezeka kwa matumizi ya mafuta ya kisukuku hakuendani na kupunguza ongezeko la joto duniani.

Muongo uliopita ndio ulikuwa na joto la kupindukia katika historia: WMO Ripoti

Tabianchi na mazingira

Muongo uliopita umethibitishwa kuwa na joto zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia, na kuendeleza mwelekeo wa kutisha wa miaka 30 amesema leo mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO akiongeza kuwa hali hiyo imechochewa bila shaka na utoaji wa gesi chafuzi kutokana na shughuli za binadamu.

Kulingana na ripoti mpya ya WMO iliyozinduliwa leo kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi unaoendelea huko Dubai Falme za nchi za Kiarabu “ikiwa ni alama ya kuvunja rekodi ya halijoto ya ardhini na baharini, muongo huo wa kati ya mwaka 2011-2020 ulishuhudia kuongezeka kwa viwango vya gesi chafuzi ambayo ilichochea upotezaji mkubwa wa barafu na kupanda kwa kiwango cha kina cha bahari.”

Ripoti hiyo inakuja wakati mkutano wa hivi karibuni wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP28, ukifikia katikati huko Dubai, ambapo nchi zimekubaliana juu ya mfuko mpya wa hiari wa kulipa fidia mataifa yaliyo hatarini kwa hasara na uharibifu kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Lakini mazungumzo magumu yanakuja katika siku zijazo kuhusu malengo ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi na kuondoa nishati ya mafuta kisukuku.

Madhara makubwa kwa Polar na maeneo ya milimani

Ripoti ya muongo wa hali ya hewa ya WMO, ambayo imezinduliwa huko Dubai, inafichua kuwa kati ya mwaka  2011 na 2020, nchi nyingi ziliripoti viwango vya juu vya joto kuliko katika muongo mwingine wowote.

Pia hupiga kengele katika "mabadiliko makubwa sana yanayofanyika katika maeneo ya ncha za dunia na milima mirefu.”

WMO inaendelea kuonya kwamba majanga ya hali ya hewa yanadhoofisha maendeleo endelevu, na athari mbaya kwa uhakika wa chakula duniani, uhamishaji na uhamiaji.

"Kila muongo tangu miaka ya 1990 imekuwa na joto zaidi kuliko ile iliyotangulia, na hatuoni dalili ya haraka ya hali hii kubadilika," ameonya Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema, na kusisitiza kwamba "Tunapoteza mbio za kuokoa barafu yetu inayoyeyuka kwa kasi. Tunapaswa kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kama kipaumbele cha juu na kikuu kwa sayari ili kuzuia mabadiliko ya tabianchi yasifurutu ada." 

Nuru ya matumaini

Ripoti hiyo inatoa picha ya kutisha, lakini pia inaangazia maendeleo chanya, ikiwa ni pamoja na kwamba juhudi za kimataifa zilizofanikiwa za kukomesha kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni chini ya Itifaki ya Montreal zimesababisha shimo dogo la ozoni la Antaktika katika kipindi cha 2011-2020.

Kwa kuongeza, maendeleo katika utabiri, mifumo ya tahadhari ya mapema, na usimamizi ulioratibiwa wa maafa umepunguza majeruhi kutokana na matukio mabaya, ingawa hasara za kiuchumi zimeongezeka, kwa mujibu wa watafiti wa WMO.

Kwa ujumla, hata hivyo, ripoti inasisitiza haja ya hatua kubwa zaidi za uhakika, wakati fedha za mabadiliko ya tabianchi za umma na za binafsi zilikaribia mara mbili kutoka 2011 hadi 2020, ongezeko mara saba ni muhimu kufikia mwisho wa muongo huu ili kufikia malengo ya tabianchi.