Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WMO yatoa wito kwa mataifa kufuatilia mzunguko wa maji ambao unazidi kuwa mbaya duniani

Familia inasafirisha chupa za maji kutoka kwenye chemchemi kufuatia uhaba wa maji nchini Lebanon.
© UNICEF/Ramzi Haidar
Familia inasafirisha chupa za maji kutoka kwenye chemchemi kufuatia uhaba wa maji nchini Lebanon.

WMO yatoa wito kwa mataifa kufuatilia mzunguko wa maji ambao unazidi kuwa mbaya duniani

Tabianchi na mazingira

Ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa, WMO inaonya kuwa kutakuweko na uhaba wa maji duniani kunatokana na vyanzo vya maji kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi, ikitaja mafuriko, joto kupindukia, ukame na kuyeyuka kwa barafu. 

Ripoti hiyo ya Hali ya Rasilimali za Maji Duniani ya 2022  inasisitiza haja ya kuelewa vyema rasilimali za maji safi na kuhimiza mabadiliko ya kimsingi ya sera. Ripoti hiyo imefafanua kuwa nchi zinahitaji ufuatiliaji ulioimarishwa, kubadilishana taarifa, ushirikiano wa mipakani, na kuongezeka kwa uwekezaji ili kudhibiti hali mbaya zaidi kwa ufanisi. 

Katibu Mkuu wa WMO Petteri Taalas, amesema ‘Ripoti hii ya WMO inatoa muhtasari wa kina, na thabiti wa rasilimali za maji duniani kote, ikionyesha ushawishi wa hali ya hewa, mazingira, na mabadiliko ya kijamii,”

Ripoti hiyo imethibitishwa na uchunguzi uliofanywa huko mashinani, utambuzi unaotegemea satelaiti, na uundaji wa kutathmini rasilimali za maji duniani, ripoti hiyo pia ina takwimu kuhusu vipengele muhimu vinayoangazia maji ya ardhini, maji kwenye hewa , vyanzo vya maji vya chemchem, mtiririko, hifadhi ya maji duniani, udongo, unyevu, maji yaliyogandishwa, uingiaji wa hifadhi, na majanga ya kihaidrolojia.

“Ripoti hii ni wito wa kuchukua hatua kwa kushirikishana taarifa ili kuwezesha kutolewa kwa maonyo ya mapema yenye maana na kwa sera zilizoratibiwa zaidi na jumuishi za usimamizi wa maji ambazo ni sehemu muhimu ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” amesema Mkuu huyo wa WMO

Ripoti hii inachanganya maoni kutoka kwa wataalam kadhaa na inakamilisha ripoti kuu ya WMO ya Hali ya Hewa Duniani.

Vijana wawili wakiwa wamebeba madumu ya maji baada ya kuteka maji kutoka kituo cha kuteka maji kilichojengwa na UNICEF na wadau wake kwenye kambi ya Bulengo magharibi mwa mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/UNI418288/Ndebo
Vijana wawili wakiwa wamebeba madumu ya maji baada ya kuteka maji kutoka kituo cha kuteka maji kilichojengwa na UNICEF na wadau wake kwenye kambi ya Bulengo magharibi mwa mji wa Goma, jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mzunguko wa maji uliovurugika

Barafu ambayp ilikuwa imefunika milima inaendelea kuyeyuka kutokana na kupanda kwa joto - na pia kuvuruga - mzunguko wa maji.

Mazingira yenye joto zaidi huhifadhi unyevu zaidi na kusababisha vipindi vizito vya mvua na mafuriko. Na kinyume chake, Mkuu huyo waWMO alisema ni maji kukauka, udongo kuwa mkavu na ukame mkali zaidi.

Kulingana na Shirika la Maji la Umoja wa Mataifa UN Water, kwa sasa, watu bilioni 3.6 wanakosa maji ya kutosha angalau kwa mwezi kwa kipindi cha mwaka mzima na hii inatarajiwa kuongezeka hadi zaidi ya bilioni tano ifikapo mwaka 2050.

Hali ilivyokuwa

Ingawa utafiti na taarifa zaidi zinahitajika, kutoka kanda kama vile Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, waandishi wa ripoti hiyo wanaamini hitimisho lililofanywa kulingana na taarifa za vituo 273 kote ulimwenguni ni suala linalopaswa kuzingatiwa moja kwa moja.

Katika eneo la utiririkaji wa maji kwenye mito na hifadhi, zaidi ya asilimia 50 ya maeneo ya vyanzo vya maji ulimwenguni na mabwawa yalionesha kutokuwa katika hali ya kawaida, ambavyo vingi vilikuwa nivikavu kuliko kawaida.

Kulikuwa na hitilafu katika unyevu wa udongo na uvukizi (uhamishaji wa maji ya nchi kavu kwenye angahewa, ama kwa uvukizi au kupitia mimea) iliyosajiliwa mwaka mzima wa 2022.

Kwa mfano, Bara la Ulaya lilipata ongezeko la uvukizi na kupungua kwa unyevu wa udongo wakati wa kiangazi. Zaidi ya hayo, ukame katika bara hilo ulileta changamoto katika mito kama vile Danube na Rhine na hata kutatiza uzalishaji wa umeme wa nyuklia nchini Ufaransa kutokana na ukosefu wa maji ya kupozea.

Ukame mkali uliathiri pia maeneo makubwa ikiwa ni pamoja na Marekani, Pembe ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bonde la La Plata huko Amerika Kusini.

Barani Asia, bonde la mto Yangtze nchini China lilikabiliwa na ukame mkubwa, huku bonde la mto Indus nchini Pakistan lilishuhudia mafuriko makubwa. Maafa hayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 1,700, huku watu milioni 33 wakiathiriwa na karibu milioni nane kuyahama makazi yao.

Hali za maji barani Afrika zinatofautiana pia. Wakati Pembe ya Afrika ilikabiliana na ukame mkali ulioathiri uhakika wa chakula wa watu milioni 21, maeneo kama vile bonde la Niger na pwani ya Afrika Kusini yalishuhudia maji kupita kiasi na mafuriko makubwa.