Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mama sayari dunia ni mmoja pekee, tufanye kila tuwezalo tumlinde- Guterres

Mtazamo wa sayari dunia kama ulivyonaswa na wanaanga wa Markani mwaka 1969
NASA
Mtazamo wa sayari dunia kama ulivyonaswa na wanaanga wa Markani mwaka 1969

Mama sayari dunia ni mmoja pekee, tufanye kila tuwezalo tumlinde- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya Mama Sayari dunia hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kufanyika kwa kila liwezekanalo kumlinda mama huyo kwa kuwa yuko mmoja tu na hakuna mbadala.
 

Guterres ametoa wito huo kupitia ujumbe wake wa video wakati huu ambapo anasema Mama Dunia anakabiliwa na majanga matatu ambayo yanahitaji udharura kuyatokomeza.

Ametaja majanga hayo matatu kuwa ni  janga la tabianchi, kutoweka kwa bayonuai na mazingira halisi na uchafuzi na taka.

“Majanga haya matatu yanatishia ustawi na uhai wa mamilioni ya watu duniani kote. Misingi ya ujenzi wa maisha yenye afya na furaha – maji safi, hewa safi na tabianchi nchi tulivu imetawanyika, na kuweka malengo yetu endelevu mashakani,” amesema Guterres.

Ametaka siku ya leo itumike kutathmini ubinadamu unatendea sayari dunia akisema ukweli ni kwamba wakaziwa dunia wamekuwa walinzi dhaifu wa nyumba yao iliyo tete.

Mlipuko wa volkano na Tsunami ya Tonga umeweka wazi mazingira hatarishi ya visiwa vidogo na Mataifa yanayoendelea (SIDS).
© Konionia Mafileo
Mlipuko wa volkano na Tsunami ya Tonga umeweka wazi mazingira hatarishi ya visiwa vidogo na Mataifa yanayoendelea (SIDS).

Kuna matumaini

Hata hivyo amesema kuna matumaini kwa kuwa miaka 50 iliyopita serikali duniani zilikutana mkutano wa kimataifa wa Stockholm ambao amesema ulikuwa ni mwanzo wa harakati za mazingira duniani.

« Tangu wakati huo, tumeona kinachowezekana tukishirikiana pamoja. Tumeweza kupunguza tundu la ozoni. Tumeongeza wigo wa ulinzi wa wanyamapori na mifumo anuwai. Tumatokomeza matumizi ya nishati chafuzi, na kuzuia mamilioni ya vizazi mfu. Na mwezi uliopita tu, tulizindua juhudi za kihistoria za kimataifa za kuzuia na kutokomeza uchafuzi utokanao na plastiki. »

Kwa pamoja tunaweza

Guterres amesema hatua hizo zimethibitisha kuwa kwa kufanya kazi pamoja binadamu wanaweza kutatua changamoto kubwa.

Amesema zaidi ya yote haki ya mazingira yenye afya inazidi kushika kasi. “Lakini tunahitaji kuchukua hatua zaidi. Na tena haraka. Hasa kuepusha janga la tabianchi.”

Ametaka hatua zaidi kuhakikisha kuwa ongezeko la joto halizidi nyuzi joto 1.5 katika Selsiyasi hivyo “serikali lazima ziwe zimepunguza uchafuzi kwa asilimia 45 ifikapo mwaka 2030, na ziache kabisa uzalishaji wa hewa ya ukaa mwaka 2050.”

Halikadhalika wachafuzi wakuu lazima wapunguze kwa kiwango kikubwa kuanzia mwaka huu. “Hii na maana kuongeza kazi ya kuachana na uraibu wa nishati kisukuku. Na kuongeza kasi ya kutumia nishati jadidifu.”

Pamoja na hatua hizo, Katibu Mkuu ametaka uwekezaji wa haraka kwenye uhimili, mnepo hususan kwa nchi masikini zaidi na zilizo hatarini ambazo zimesababisha kidogo janga hili.

UN News Kiswahili
Mikoko Pamoja yaleta manufaa Gazi Bay

Mwelekeo ni Stockholm + 50

Mwezi Juni, dunia inakutana tena Sweden kwa jili ya miaka 50 tangu mkutano wa Stockholm na ndio maana Katibu Mkuu Guterres anataka kila mtu ahakikishe “viongozi wetu wanakuja na hatua za kijasiri kutatua majanga matatu ya dharura ya sayari dunia. Kwa sababu tuna Mama Sayari dunia mmoja. Tufanye kila tuwezalo kumlinda.”