Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya watu duniani itafikia bilioni 8 tarehe 15 Novemba 2022. DRC na Tanzania zatajwa 

Watu wakitembea katika maduka jijini Kampala, Uganda
IMF/Esther Ruth Mbabazi
Watu wakitembea katika maduka jijini Kampala, Uganda

Idadi ya watu duniani itafikia bilioni 8 tarehe 15 Novemba 2022. DRC na Tanzania zatajwa 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ripoti ya mwaka huu 2022 ya Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani  iliyotolewa leo na Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na masuala ya kijamii, UNDESA, imebainisha kuwa idadi ya watu duniani inakadiriwa kufikia bilioni 8 ifikapo tarehe 15 Novemba mwaka huu 2022.

Ripoti hii ya  Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani iliyotolewa hii leo katika Siku ya Idadi ya Watu Duniani, ni toleo la ishirini na saba la makadirio rasmi ya idadi ya watu ya Umoja wa Mataifa ikitoa makadirio ya idadi ya watu kuanzia mwaka 1950 hadi sasa.

 Tathmini hii ya hivi karibuni, inazingatia matokeo ya sensa 1,758 za kitaifa zilizofanywa kati ya mwaka 1950 na 2022, pamoja na taarifa kutoka katika mifumo muhimu ya usajili na kutoka kwa sampuli 2,890 wakilishi za kitaifa kutoka maeneo au mataifa 237 duniani. 

Taarifa kwa waandishi wa habari  iliyotolewa hii leo jijini New York, Marekani  ikidokeza kwa ufupi yaliyomo katika ripoti hiyo ya matarajio ya ongezeko la watu, imeanza kwa kueleza kuwa inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka kesho yaani 2023, India itaipita China kwa kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani. 

Taarifa hiyo imemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisema, "Siku ya Idadi ya Watu Duniani mwaka huu inakuja wakati wa mwaka muhimu, wakati tunatarajia kuzaliwa kwa mkazi wa bilioni nane wa Dunia. Hili ni tukio la kusherehekea utofauti wetu, kutambua ubinadamu wetu wa pamoja, na kustaajabia maendeleo ya afya ambayo yameongeza muda wa maisha na kupunguza kwa kiasi kikubwa viwango vya vifo vya watoto na wakati wa kujifugua. Wakati huo huo, ni ukumbusho wa uwajibikaji wetu wa pamoja. kutunza sayari yetu na muda wa kutafakari ni wapi bado tunakosa kutimiza ahadi zetu sisi kwa sisi. Wakati huo huo, ni ukumbusho wa uwajibikaji wetu wa pamoja kutunza sayari yetu na muda wa kutafakari ni wapi bado tunakosa kutimiza ahadi zetu sisi kwa sisi.” 

Aidha utafiti umeonesha Idadi ya watu duniani inaongezeka kwa kasi ndogo zaidi tangu mwaka 1950, ikiwa imeshuka chini ya asilimia 1 mwaka 2020 lakini idadi ya watu duniani inaweza kuongezeka hadi kufikia bilioni bilioni 9.7 mwaka 2050 na kufikia karibu watu bilioni 10.4 katika miaka ya 2080 na kubaki katika kiwango hicho hadi mwaka 2100. 

Vilevile taarifa imeweka wazi kuwa zaidi ya nusu ya matarajio ya ongezeko la idadi ya watu duniani hadi mwaka 2050 litakuwa katika nchi nane ambazo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Misri, Ethiopia, India, Nigeria, Pakistani, Ufilipino na Tanzania. Nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zinatarajiwa kuchangia zaidi ya nusu ya ongezeko la watu linalotarajiwa linalotarajiwa kufikia mwaka 2050.