Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres alaani vikali shambulio lililokatili maisha ya walinda amani wawili Mali 

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Guterres alaani vikali shambulio lililokatili maisha ya walinda amani wawili Mali 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio la jana la Kilipuzi cha mabomu (IED) dhidi ya msafara wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali (MINUSMA), ambapo walinda amani wawili kutoka Misri waliuawa na wengine tisa walijeruhiwa.  

Katika ujumbe wake uliotolewa na msemaji wake mjini New York Marekani, Bwana Guterres amesema shambulio hilo lilitokea takriban kilomita 62 kaskazini Mashariki mwa mji wa Gao, ulioko kaskazini mwa Mali. 

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha, na pia kwa serikali na watu wa Misri, ambao wanajeshi wao wanaendelea kulipa gharama kubwa zaidi katika huduma ya ulinzi wa amani nchini Mali, na mareruhi wote amewatakia ahueni ya haraka. 

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa mashambulizi yanayolenga walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa. 

Walinda amani wa MINUSMA akiwa kwenye doria huko Gao nchini Mali
/Marco MINUSMADormino
Walinda amani wa MINUSMA akiwa kwenye doria huko Gao nchini Mali

Ametoa wito kwa mamlaka ya mpito nchini Mali kufanya kila juhudi katika kuwabaini wahusika wa shambulio hilo na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo. 

Guterres ametoa pongezi kwa walinda amani wa MINUSMA , ambao amesema azma na ujasiri wao ni mfano wa kuigwa , na kwamba wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu sana wakiunga mkono watu wa Mali.