Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mchango wa wanawake kwenye ulinzi wa amani una thamani kubwa:Guterres

Wakili wa Jinsia wa Jeshi la Wanajeshi anatambua kujitolea kwa bidii ya kila mtu anayetunza amani katika kukuza kanuni za Azimio la Usalama la Umoja wa Mataifa 1325 juu ya Wanawake, Amani na Usalama.
UN
Wakili wa Jinsia wa Jeshi la Wanajeshi anatambua kujitolea kwa bidii ya kila mtu anayetunza amani katika kukuza kanuni za Azimio la Usalama la Umoja wa Mataifa 1325 juu ya Wanawake, Amani na Usalama.

Mchango wa wanawake kwenye ulinzi wa amani una thamani kubwa:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mchango wa wanawake walinda amani mkubwa sana hivyo unapaswa kuenziwa kwa kuongeza idadi wanawake hao katika operesheni za ulinzi wa amani.

 

Katibu Mkuu ameyasema hayo katika ujumbe wake kuelekea siku ya walinda amani duniani ambayo kila mwaka hufanyika Mei 29.

Katika ujumbe hu amesema “Leo hii tunawatunuku zaidi ya wanaume na wanawake milioni moja na ambao wamejitolea kufanya kazi ya ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa pamoja na zaidi ya watu 3,900 ambao wamepoteza maisha yao wakati wakitekeleza majukumu yao. Pia tunawashukuru zaidi ya raia 95,000, wahudumu kutoka polisi na jeshi wanaofanya kazi hizo duniani kote.”

Guterres amesema walinda amani hao wanakabiliwa na moja ya changamoto kubwa zaidi ya kujitolea kwenye majukumu yao ya kulinda amani wakati huohuo wakishughulikia changamoto za janga la virusi vya corona au COVID-19.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “wanawake na ulinzi wa amani” ambayo  inaainisha umuhimu wao wa kipekee katika shughuli za kulinda amani.

Bwana. Guterres ameongeza kuwa “Wanawake kwa kawaida huwa na nafasi kubwa zaidi ya kufikia jamii tunazozitumikia, hali hii hutuwezesha kuboresha ulinzi wa raia, kuendeleza haki za binaadamu na kuboresha utekelezaji kwa ujumla. Hii ina umuhimu zaidi wakati huu, ambapo walinzi wa amani wanawake wako mstari wa mbele kusaidia mwitikio wa kushughulikia COVID-19 katika jamii ambazo tayari ni dhaifu kwa kutumia redio za jamii kueneza jumbe zinazohusu afya ya umma, kwa kuwasilisha mahitaji maalumu kwa jamii ili wajizatiti, na kusaidia jitihada za wajenga amani ambao ni raia.”

 

Mchango wa wanawake una thamani kubwa katika ulinzi wa amani

 

 Hata hivyo, Katibu Mkuu amesema wanawake wanaendelea kuwasilisha asimia 6 tu ya wanajeshi na polisi wanaovaa magwanda, watumishi wa utawala wa sheria na maafisa warekebishaji  wa tabia wanaofanya kazi kwenye ulinzi wa amani.

Ameongeza kuwa wakati huu tukiadhimisha miaka 20 ya azimio la Baraza la Usalama lenye kumbukumbu nambari 1325 linalohusu Wanawake, amani na ulinzi, tunapaswa tufanye juhudi zaidi kufikia usawa wa uwakilishi wa wanawake katika nyanja za amani na ulinzi.

Na kwa mantiki hiyo amesema “Pamoja, tuendeleze jitihada za kuleta amani, kushinda baa hili na kujenga maisha bora ya baadae.”