Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO inasema janga la kiafya linashika kasi Congo DRC

WHO inasema janga la kiafya linashika kasi Congo DRC

Pakua

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC iko katikati ya janga la kiafya linaloongezeka limeonya leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO  na kusisitiza kwamba magonjwa ya milipuko yamezorotesha sana hali nchini humo katika miezi ya hivi karibuni kutokana na ghasia na mafuriko. 

Kulingana na WHO, DRC imekabiliwa na ongezeko la migogoro na ghasia, na kusababisha watu wengi kukimbia makazi yao, magonjwa kuenea, unyanyasaji wa kijinsia, na kiwewe kikubwa cha akili, haswa mashariki mwa nchi hiyo.

Dkt. Adelheid Marschang, Afisa wa Dharura wa WHO, ameuambia mkutano wa waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva kwamba "Kutokana na hali hiyo, watu wanakabiliwa na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu, surua, uti wa mgongo, ndui na tauni, yote yakichangiwa na mafuriko makubwa na maporomoko ya ardhi yanayoathiri sehemu kadhaa za nchi hiyo."

Tangu mwanzoni mwa mwaka, WHO inasema zaidi ya visa 20,000 vya kipindupindu vimerekodiwa, viki katika eneo la Kivu Kaskazini.

Pia kumekuwa na zaidi ya wagonjwa  65,000 wa surau na vifo 1,523, huku idadi halisi ikiwezekana kuwa kubwa zaidi kutokana na kutofuatilia na kuripoti magonjwa kwa kiasi cha kutosha. Wakati huo huo, kumekuwa na kesi 3,073 za homa ya uti wa mgongo ikiwa ni pamoja na vifo 251vilivyoripotiwa katika  katika nchi hii ya Maziwa Makuu.

WHO pia imekuwa na wasiwasi juu ya lahaja ya mpox katika miezi ya hivi karibuni ambapo zaidi ya kesi 11,000 zikijumuisha vifo 445 zimerekodiwa, na kukiwa na kiwango cha juu cha vifo vya zaidi ya asilimia 4. Watoto wameelezwa kuathiriwa zaidi na janga hili, na viwango vya juu zaidi vya vifo.

Migogoro ya silaha na watu kuhama makazi yao vimetajwa kuwa ni vichocheo vikuu vya uhaba wa chakula.

WHO inasema takriban asilimia 40 ya watu ambayo ni sawa na watu milioni 40 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula nchini DRC na, watu milioni 16 kati yao wako katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa chakula. Jumla ya watu milioni 25 nchini humo wanategemea msaada wa kibinadamu kuweza kuishi na kuifanya DRC kuwa sasa ndiyo nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu duniani.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'29"
Photo Credit
© WFP/Benjamin Anguandia