Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi ya mwanamke aliyebakwa na kupata ujauzito wakati wa mzozo Sudan

Simulizi ya mwanamke aliyebakwa na kupata ujauzito wakati wa mzozo Sudan

Pakua

Mwaka mmoja wa mzozo nchini Sudan umewafanya wananchi wengi kukimbia maeneo waliyokuwa wakiishi kusaka hifadhi pamoja na kukimbilia nje ya nchi. Pamoja ya kukimbia vita lakini pia wanasalia na majeraha ndani ya mioyo yao kutokana na masahibu waliyopitia. Mmoja wao ni Bi. Fatima ambaye alibakwa na kupata ujauzito. 

Fatima sio jina lake halisi, tunalitumia hili ili kuficha utambulisho wake na hapa anaanza kueleza yale yaliyomsibu akiwa mikononi mwa wanamgambo wenye silaha.

“Nilibakwa mara tatu. Aliniambia lala chini, usipotaka kulala chini naweza kukuuwa. Sijui sasa kama ni huyo mwanaume aliniingilia mara tatu au kulikuwa na wengine.” 

Akiwa na kiwewe na aliyekata tamaa, Fatima akaukimbia mji wake wa Khartoum akiwa na watoto wake kwenda kusini mashariki mwa Sudan, kusaka hifadhi na alipofika huko, anasema “Nilikwenda kuripoti tukio hilo katika kliniki na kusaka msaada ili waweze kunifanyia uchunguzi wa jumla. Nikaenda hospitalini na kila kitu kilikuwa sawa. Baada ya miezi miwili nilienda tena kliniki na wafagundua kuwa nina ujauzito.”

Pole sana Fatima, sasa ni nini unachohitaji wakati huu nchi yako bado ingali vitani? 

“Tunahitaji amani kwa ajili yetu, ili tuweze kurudi na kuishi nchini Sudan.”

Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kama vile UN WOMEN, OCHA, UNHCR na hata Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili wa Kingono kwenye mizozo wamekuwa wakipazia unyanyasaji wa kijinsia nchini Sudan huku wakieleza wasiwasi wao mkubwa kuwa ukubwa halisi wa mgogoro bado haujajulikana na kumekuwa na viwango vidogo vya kuripoti matukio ya kikatili kwani baadhi ya wanawake na wasichana wanaogopa unyanyapaa na kutokuwa na imani na taasisi za kitaifa.

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'2"
Photo Credit
©UNHCR/Ruben Salgado Escudero