Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi kutoka Sudan wanoingia Sudan Kusini wanaendelea kuongezeka

Wakimbizi kutoka Sudan wanoingia Sudan Kusini wanaendelea kuongezeka

Pakua

Tarehe 15 April wiki ijayo siku ya jumatatu nchi ya Sudan itatimiza mwaka mmoja rasmi tangu kuanza kwa mzozo kati ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na Vikosi vya jeshi la Sudan (SAF). Vita hiyo imesababisha maelfu ya watu kuwa wakimbizi wa ndani na wengine kusaka hifadhi nchi Jirani. Mashirika ya misaada ya kibinadamu nayo yamekuwa mstari wa mbele kusaidia wananchi wenye uhitaji japo yanakabiliwa na ufinyu wa bajeti.

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP inaanza kwa kuonesha wananchi wakiwa na vifurushi mikononi, wengine wakiwa wamepanda usafiri unaosukumwa na ngombe na wengine mabasi wakiingia katika mpaka wa Joda nchini Sudan kusini wakitokea nchini Sudan.

“Tumesafiri kwakutumia basi na imetuchukua siku mbili kufika hapa”, ndivyo anavyosema Hamida Ibrahim mkimbizi kutoka Sudan. Anaendelea kwa kueleza kile wanachohitaji kwa sasa. 

“Tunahitaji chakula. Huo ndio msaada wa haraka tunaohitaji ili tuweze kuishi. Kwa sababu tupo na watoto na hawana uwoga wanachojua wanakuja hapa kufata usalama” 

Kiongozi wa WFP katika eneo hili Leonidace Rugemalila anasema mzozo huu wa Sudan umemuathiri kila mtu.

“Katika kipindi cha miezi mitatu idadi ya watu wanaovuka mpaka huu kila siku imeongezeka kutoka watu 1,500 mpaka takriban watu 2,500.”

Naye Mkuu wa lishe Aachal Chand anasema wengi wa waaathirika wa mzozo nchini Sudan ni wanawake na watoto, na walioathirika zaidi ni wajawazito, wanawake wanaonyonyesha na watoto wenye umri chini ya miaka mitano. 

“Wanapovuka mpaka, mtu yeyote mwenye umri zaidi ya miaka mitano anapatiwa biskuti za lishe kama chakula cha haraka chakumpa lishe. Kwa watoto chini ya miaka mitano tunawapa chakula maalum cha lishe. Kuanzia saa mbili asubuhi mpaka wakati huu saa 10 jioni wameshatoa lishe kwa takriban watoto 400 ambao wamepokea matibabu ya utapiamlo au huduma za matibabu.”

Chand ameeleza kuwa WFP na wadau wake wanaendelea kutoa msaada hata hivyo wanakabiliwa na ufinyu wa bajeti.

“Watu wanahitaji msaada wa afya na lishe, watu wanahitaji usaidizi katika kupata uhakika wa chakula, watu wanahitaji msaada wa kuweza kuwasaidia kufika katika maeneo wanayotaka kuelekea.Sudan na athari zake kwa nchini ya Sudan Kusini zinasahaulika na tunatakiwa kuhakikisha hatusahau mzozo huu kwasababu hawa ni watu na wanapata athari halisi katika maisha yao.” 

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'42"
Photo Credit
© WFP/Hugh Rutherford