Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mbinu za medani tulizopatiwa ni za kimataifa- Afisa FARDC

Mbinu za medani tulizopatiwa ni za kimataifa- Afisa FARDC

Pakua

Siku zikizidi kuhesabiwa kwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, kuondoka nchini humo, ujumbe huo unaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujengea uwezo jeshi la serikali, FARDC kuweza kukabili vikundi vilivyojihami ambavyo vinatajwa kuhusika na asilimia 65 ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo mwezi Februari mwaka huu, kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya Umoja wa Mataifa na serikali. Je, FARDC linajengewa uwezo gani? Assumpta Massoi anafafanua zaidi.

Hapa si uwanja wa vita bali ni uwanja wa mazoezi! Wanajeshi 30 wa FARDC au jeshi la serikali nchini DRC wakiwa kwenye mafunzo  ya  kulenga shabaha. Mbele kuna karatasi lililochorwa binadamu na sasa wanatakiwa kulenga maeneo mbali mbali ya mwili yaliyowekwa alama.

Ni mbinu wanazopatiwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Brazil, hapa Beni jimboni Kivu Kaskazini ili waweze kukabiliana na waasi kwenye maeneo misituni. Kapteni Rombaut Mukoka ni Afisa wa jeshi la FARDC na anasema, “Mafunzo haya ni muhimu sana. Yanapaswa kuendelea ili hatimaye wanajeshi wetu waweze kunufaika. Hizi mbinu walizojifunza ni mpya sana kwetu na zinatambulika katika medani za kimataifa.”

Mafunzo ya kulenga shabaha yanaendelea na kisha mkufunzi kutoka Brazil anajongea kwenye picha ile akiwa na mmoja wa wanafunzi ili kuonesha ni wapi haswa wanapaswa kulenga.

Jenerali Luciano Alfred Matamba ni Mkuu wa kikosi cha kujibu mashambulizi, FIB cha MONUSCO mjini Beni na anafafanua lengo la mafunzo hayo yaliyofanyika kwa wiki tatu.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwapatia mbinu na ufundi za kuendesha operesheni msituni. Kama unavyofahamu hapa Kivu Kaskazini tuko kwenye eneo la operesheni ambalo kwa kiasi kikubwa ni pori na mashambulizi yanayofanywa na waasi wa ADF yanahitaji mbinu mtu kuwa na hizo mbinu za kupigana msituni. FARDC [EF EI AR DE SE] ni wadau wetu ambao tunapaswa kushirikiana nao kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa namba 2717 [Mbili Saba Moja Saba]. Ni pale tu ambapo tutajifunza pamoja na kuwa na mbinu sawa ndio tutaweza kutatua matatizo yaliyoko hapa.”

Audio Credit
Evarist Mapesa
Audio Duration
2'12"
Photo Credit
MONUSCO/Ado Abdou