Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN - Bila usitishaji mapigano hali ya kibinadamu inaendelea kuwa tete Gaza

UN - Bila usitishaji mapigano hali ya kibinadamu inaendelea kuwa tete Gaza

Pakua

Mashirika ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo kwa mara nyingine yameonya kwamba bila dalili zozote za usitishaji mapigano Gaza hali ya kibinadamu inaendelea kuwa janga huku mashambulizi ya Israel yakiendelea kukatili maisha, kufurusha watu na kusababisha uharibifu usioelezeka na njaa nayo ikiongeza hofu ya hatma ya watu wa eneo hilo. 

Asante Anold kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA usiku wa kuamkia leo makombora ya Israel yameendelea kuvurumishwa kuelekea Gaza Kaskazini, Khan Younis na Rafah ambako takriban Wapalestina milioni 1.2 sasa wanaishi katika makazi rasmi na yasiyo rasmi na hivyo kuwaongezea hofu ya mustakbali wa maisha yao.

Pia shirika hilo linasema fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wenye uhitaji mkubwa bado ni mtihani hasa kutokana na mamlaka ya Israel kuendelea kulinyima vibali shirika la UNRWA kufikisha msaada muhimu wa chakula na mahitaji mengine hasa Gaza Kaskazini.

Hatua hiyo kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA imezidisha njaa kwa watu ambao tayari wako taaban na mapigano yanayoendelea. 

Tangu Machi mosi OCHA inasema Israel imekataa kuruhusu asilimia 30 ya operesheni za kibinadamu Gaza Kaskazini na kuathiri kwa kiasi kikubwa operesheni za UNRWA.

Watoto 27 wameripotiwa kufa njaa kutokana na utapiamlo hadi sasa huku shirika la Kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF likionya kwamba Maisha ya maelfu wengine yako hatarini ukizingatia ukweli kwamba tangu Oktoba 7 mwaka jana watoto zaidi ya 13,000 wameuawa kutokana na vita inayoendelea lakini njaa nayo ni tishio kubwa.

Kuhusu uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na vita inayoendelea ripoti ya pamoja ya tathimini ya Umoja wa Mataifa na Benk ya Dunia iliyotolewa leo inasema uharibifu huo unakadiriwa kuwa takriban dola bilioni 18.5 ambao ni sawa na asilimia 97 ya pato la taifa la Ukingo wa Magharibi na Gaza kwa mwaka 2022.

Na hapa Makao Makuu leo Umoja wa mataifa umepokea barua rasmi kutoka kwa mamlaka ya Palestina ikiomba kuwa mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa badala ya nafasi ya uangalizi iliyonayo sasa. 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'31"
Photo Credit
© UNRWA