Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa yataka nchi kuwa na makubaliano ya ushirikiano wa matumizi ya vyanzo vya maji

Umoja wa Mataifa yataka nchi kuwa na makubaliano ya ushirikiano wa matumizi ya vyanzo vya maji

Pakua

Leo ni siku ya maji duniani chini ya kauli mbiu Maji kwa amani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii amehimiza nchi kuhakikisha zinashirikiana na kuwa na makubaliano ya kutumia vyanzo vya maji. 

Katika ujumbe wake huo Guterres ameeleza kuwa mpaka sasa ulimwenguni “Nchi 153 zinashirikiana vyanzo vya maji lakini ni nchi 24 pekee zenye makubaliano kwa vyanzo vyao vyote vya maji wanavyoshirikiana.” 

Amesema hali haipaswi kuwa hivyo na nchi zinatakiwa “kutekeleza Mkataba wa Maji wa Umoja wa Mataifa ambao lengo lake ni kuhamasisha usimamizi wa rasilimali za maji za pamoja kwa njia endelevu.”

Hii leo kukiwa na mikutano mbalimbali pamoja na ripoti za mashirika ya Umoja wa Mataifa, kimataifa, kitaifa na asasi za kiraia zinazoelezea matumizi ya maji pamoja na changamoto zake ulimwenguni, Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka watu wote kutambua kwamba kushirikiana katika kulinda vyanzo vya maji kunaweza kuimarisha na kudumisha amani. 

Kama Kauli mbiu ya mwaka huu inavyosema “Maji kwa amani” Guterres amesema “Hatua zinachokuliwa kwa ajili ya maji ni hatua kwa ajili ya amani na hii inahitajika zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Usimamizi wa maji unaweza kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na uhusiano kati ya jamii, na kujenga uwezo wa kukabiliana na majanga yaletwayo na mabadiliko ya tabianchi. Unaweza pia kuendeleza maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu SDGs ambayo ni msingi wa jamii zenye amani, ikiwa ni pamoja na kuboresha afya, kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa, na kuimarisha usalama wa chakula na maji.

Amehitimisha kwa kutoa wito kwa jamii yote kujitolea kufanya kazi pamoja, kufanya maji kuwa nguvu ya ushirikiano, maelewano na utulivu, na hivyo kusaidia kuunda ulimwengu wa amani na ustawi kwa wote.

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
1'57"
Photo Credit
UNEP/Lisa Murray