Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto Charles: MONUSCO imenitoa msituni, asanteni sana

Mtoto Charles: MONUSCO imenitoa msituni, asanteni sana

Pakua

Harakati za ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, za kuondoka nchini humo zikiendelea, tunamulika hatua chanya zilizochukuliwa na ujumbe huo katika kunusuru vijana waliokuwa wanatumikishwa na waasi mashariki mwa nchi hiyo.

Miongoni mwao ni Charles, mwenye umri wa miaka 16 ambaye si jina lake halisi. Yeye alitumikishwa msituni na waasi kwa kipindi cha miaka miwili.

Akizungumza huku sura yake ikiwa imefichwa kwenye video ya MONUSCO, Charles anakumbuka kuwa walikuwa shambani wanalima wakati waasi wa Mai Mai walipofika na kuwakamata.

“Walitueleza kuwa hawana watu wa kuwasaidia mapigano hivyo wakatuchukua. Tulipofika walituona kuwa tuna mawazo ya kutoroka hivyo walitufungia ndani kwa wiki tatu,” anasema Charles.

Anasema walipotoka fikra za kutoroka zikatoweka, wakafundishwa kupigana msituni na walipigana mara sita. Lakini haikuwa rahisi kwani wenzake 12 waliuawa huku porini wakati wa mapigano huku yeye mwenyewe akishuhudia.

“Niliumia sana. Chakula nacho kilikuwa shida kupata, maisha yalikuwa magumu mno. Nikafikiria nikaona bora nirejee kwa familia yangu.’

Walichofanya yeye na wenzake, usiku wa saa saba walitoroka hadi mji wa jirani ambako huko walijisalimisha kwa kiongozi mmoja na kumweleza kuwa wamechoka kuishi na kupigana porini.

Kiongozi huyo aliwachukua na kuwapeleka Beni, mji ulioko jimboni Kivu Kaskazini.

Charles anasema kiongozi huyo aliwasaidia kuwakutanisha na shirika la kiraia la ACOPE, mdau wa MONUSCO. Hapo walipata mafunzo kwa wiki tatu ikiwemo utengenezaji majiko banifu yasiyochafua mazingira.

“Sasa maisha ni mazuri hapa na wito wangu kwa wale watoto na vijana walioko msituni wakipigana ni kwamba waondoke huko waache kupigana, waje wajisalimishe kwa serikali ili waweze kujiendeleza.”

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'19"
Photo Credit
©TANZBATT 9 / Private Sosper Msafiri