Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Umoja wa Mataifa hauondoki Sudan

Guterres: Umoja wa Mataifa hauondoki Sudan

Pakua

Ikiwa leo ndio siku ya mwisho ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia kipindi cha mpito nchini Sudan (UNITAMS), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema pamoja na kwamba UNITAMS inaondoka Sudan lakini Umoja wa Mataifa hauondoki nchini humo na unaendelea kujitolea kwa dhati kutoa usaidizi wa kibinadamu wa kuokoa maisha na kusaidia watu wa Sudan katika matarajio yao ya mustakabali wenye amani na usalama. 

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wake usiku wa jana Februari 28 saa za New York, Marekani, Katibu Mkuu Guterres ameanza kwa kurudia shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi wote wa kimataifa na kitaifa wa UNITAMS kwa kujitolea kwao na huduma kwa watu wa Sudan katika muda wote wa majukumu ya Ujumbe huo.

Stéphane Dujarric ambaye ni Msemaji wa Katibu Mkuu anaeleza kwamba timu ndogo itasalia mjini Port Sudan ili kusimamia mchakato mzima wa makabidhiano kuanzia tarehe 1 Machi na kwamba Katibu Mkuu anategemea ushirikiano kamili wa mamlaka ya Sudan ili kuhakikisha mchakato huu unakamilika kwa urahisi na haraka iwezekanavyo.

Mzozo unaoendelea kupamba moto nchini Sudan unazidi kudidimiza utawala wa sheria na ulinzi wa raia na kuhatarisha nchi nzima na eneo zima. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatoa wito kwa pande zinazozozana kuweka chini silaha zao na kujitolea kwa mazungumzo mapana ya amani yatakayosababisha kuanzishwa tena kwa mpito wa kidemokrasia unaoongozwa na raia.

Wazo la kutaka UNITAMS ifungwe lilitoka kwa mamlaka za Sudan na baadaye mwishoni mwa mwaka jana, Baraza la Usalama liliridhia ombi hilo na kupitisha azimio.

Mjumbe Binafsi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Sudan, Ramtane Lamamra, ameanza kazi yake ya kuunga mkono juhudi za upatanishi, kwa uratibu na ushirikiano wa karibu na wadau wa Afrika na wengine wa kimataifa. Juhudi hizi za upatanishi zitakamilisha kazi muhimu inayoendelea ya Timu ya Nchi ya Umoja wa Mataifa mashinani, ambayo ni pamoja na kutoa usaidizi wa kibinadamu wa kuokoa maisha. Katibu Mkuu anatoa wito kwa mamlaka za Sudan kuendeleza ushirikiano wao, ikiwa ni pamoja na kuwezesha utoaji wa visa ya kuingia kwa wakati na kutowawekea vikwazo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wadau nchini humo kutoa msaada unaohitajika.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
1'57"
Photo Credit
UN Photo/Evan Schneider (Maktaba)