Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO/UNHCR: Asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza

WHO/UNHCR: Asilimia 75 ya vifo vyote duniani vinatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Pakua

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani WHO  na la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR leo yameonya kwamba athari zinazoletwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile saratani, magonjywa na mfumo wa hewa na kisukari kwa maisha ya watu duniani ni kubwa huku yakiwa ni chanzo cha asilimia 75 ya vifo vyote. 

Katika tarifa yao ya pamoja iliyotolewa mjini Geneva Uswis kwa mashirika hayo yamesema Watu walioathiriwa na dharura za kibinadamu wako katika hatari zaidi ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza NCDs huku ikikadiriwa kuwa magonjwa ya kiharusi na shinikizo la damu  yana uwezekano wa kuongezeka mara tatu zaidi kunapokuwa na majanga ya kibinadamu.

Hata hivyo, yameongeza kuwa huduma na matibabu ya NCDs mara nyingi havijumuishwi kama sehemu ya kawaida ya maandalizi ya hatua za dharura ya kibinadamu, ambayo huzingatia mahitaji ya haraka zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema. "Watu wanaoishi na NCDs katika majanga ya kibinadamu wana uwezekano mkubwa wa kuona hali zao zikiwa mbaya zaidi kutokana na kiwewe, msongo wa mawazo, au kutoweza kupata dawa au huduma. Mahitaji ni makubwa, lakini rasilimali hazitoshi. Lazima tutafute njia za kuunganisha vyema huduma za NCD katika kukabiliana na dharura, ili kulinda maisha zaidi kutokana na majanga haya yanayoweza kuepukika na kuboresha usalama wa afya."

Wakimbizi wametajwa kwamba mara nyingi wanakabiliwa na ukosefu wa huduma za afya, kutokana na hali mbaya ya maisha, matatizo ya kifedha, na hali mbaya ya kisheria.

Filippo Grandi,ambaye ni  Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Wakimbizi amesema "Kadiri watu wanaofurushwa makwao wanavyoongezeka, lazima tufanye kazi ili kuhakikisha haki ya afya ya wakimbizi, watu wengine waliolazimika kukimbia na jamii zinazowapokea. Ni muhimu kwamba sera, na rasilimali ziwepo ili kusaidia kujumuishwa kwa wakimbizi katika mifumo ya afya ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kupata huduma za magonjwa yasiyoambukiza. Lazima tuwe wabunifu, na kufanya kazi na serikali na washirika kutatua changamoto kama hizi."

NCDs zilichangia asilimia kubwa ya vifo vyote katika nchi zinazotoa wakimbizi wengi wanaosaidiwa na UNHCRambapoasilimia 75 Syria, asilimia 92 nchini Ukraine, asilimia 50 nchini Afghanistan na asilimia 28 Sudan Kusini.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'40"
Photo Credit
© WHO/ Blink Media/Neil Nuia