Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres: Tunahitaji utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu

Guterres: Tunahitaji utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo katika mkutano wa usalama unaofanyika mjini Munich Ujerumani ametoa wito wa kuwepo utaratibu wa kimataifa ambao unafanya kazi kwa kila mtu. 

Asante Evarist Guterres katika hotuba yake amesisitiza wito huo wa amani na utaratibu wa kisasa wa kimataifa akisema utaratibu wa leo wa kimataifa haufanyi kazi kwa kila mtu, "Kwa kweli, ningeenda mbali zaidi na kusema kwamba haufanyi kazi kwa mtu yeyote." 

Akielezea hali ya kimataifa, Katibu Mkuu  amesema  hivi sasa dunia inakabiliwa na changamoto lukuki, lakini jumuiya ya kimataifa imegawanyika zaidi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka 75 iliyopita.

Amesisitiza kwamba "Leo hii tunashuhudia nchi zikifanya chochote wapendacho, bila uwajibikaji." 

Ameonya kwamba “Kama Ripoti ya Usalama ya Munich inavyoweka bayana mafanikio ya jamii kupitia ushindani kati ya nchi yanapewa kipaumbele badala ya kuangalia faida kwa wote, kupitia ushirikiano”. 

Ripoti ya Usalama ya Munich huchapishwa kila mwaka kabla ya mkutano na kuchambua masuala muhimu ya sera ya usalama.

Guterres ameongeza kuwa migogoro inaongezeka, inayohusishwa na ushindani na kutokujali.

Hivyo amesisitiza kuwa utaratibu wa kimataifa ambalo linafanya kazi kwa kila mtu lazima lishughulikie mapungufu haya na kutoa suluhisho.

"Ikiwa nchi zingetimiza wajibu wao chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kila mtu duniani angeishi kwa amani na utu".

Katibu Mkuu amegusia pia migogoro inayoendelea duniani mathalan amesema hali ya Gaza ni janga la kutisha la mkwamo katika uhusiano wa kimataifa.

Hakuna kinachoweza kuhalalisha mashambulizi ya kiholela yaliyoanzishwa na Hamas tarehe 7 Oktoba, Guterres amesisitiza kwa wakuu wa nchi na serikali kutoka duniani kote mjini Munich na kuongeza kuwa “Na hakuna kinachoweza kuhalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina katika hatua za kijeshi za Israeli.

Mashambulizi ya kila upande dhidi ya mji wa Gaza yatakuwa mabaya kwa raia wa Palestina ambao tayari wako kwenye zahma kubwa, ameonya Guterres katika hotuba yake kwa washiriki wa ngazi za juu wa mkutano huo.

Masuala mengine aliyozungumzia ni mkutano wa siku zijazo ambao utafanyika Septemba kmwa huu ambapo amesema “tunahitaji kuimarisha usanifu wa amani na usalama wa kimataifa ili kukabiliana na vitisho na changamoto za leo, kama vile mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi, akili bandia au akili mnemba, au kutumia mtandao kama silaha.”

Na Jana Alhamisi, siku moja kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Usalama wa Munich, Guterres alitembelea sinagogi la "Ohel Jakob"

ambako kuna majina ya Wayahudi zaidi ya 4,500 wa Munich ambao waliuawa wakati wa enzi ya Manazi na kusistiza kuwa chuki dhidi ya Wayahudi inapaswa kukomeshwa kote duniani.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'40"
Photo Credit
MSC/Marc Muelle