Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF Rwanda inaboresha maisha ya watoto wenye ulemavu wa kusikia

UNICEF Rwanda inaboresha maisha ya watoto wenye ulemavu wa kusikia

Pakua

Ruzuku inayotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini Rwanda kwenye vifaa vya kusaidia watoto kuweza kusikia vyema imeleta manufaa na kurudisha ndoto za watoto waliokuwa na changamoto ya kusikia. Leah Mushi anatueleza kuhusu mmoja wa watoto wanufaika. 

Huyu ni Pascaline Uwababyeyi mwanafunzi wa shule ya msingi nchini Rwanda anasema kabla ya kupata vifaa vya kumsaidia kusikia vyema alikuwa hawezi kucheza na watoto wenzake kwani hakuweza kuwasikia kile walichokuwa wakisema. Lakini sasa anaweza kucheza nao kwani anawasikia vyema kabisa.”

Pascaline ni mmoja wa wanufaika wa ruzuku inayotolewa na UNICEF nchini Rwanda katika vifaa vya kusaidia kusikia vizuri ambavyo vimepunguzwa bei kwa zaidi ya asilimia 94 kutoka dola 2000 mpaka dola 118. 

Mama yake Pascaline Bi. Appoline Uwababyeyi anasema anaona mabadiliko katika maisha ya mwanae.

“Kitu kipya nilichokiona kutoka kwa mwanangu ni kwamba sasa anafurahia kusoma zaidi kuliko hapo awali. Anapofika darasani, anaweza kusikia, ilhali hapo awali, hakuweza na angeogopa kuuliza maswali, alikuwa ananiambia "Nikiuliza, watanicheka." Lakini sasa, mwalimu anapoeleza jambo lililoandikwa ubaoni, yeye husikia na kuelewa, kama tu wanafunzi wenzake wote.”

Pascaline anaeleza faida alizozipata baada ya kuanza kuvaa kifaa cha kumsaidia kusikia vizuri kuwa sasa anaweza kusikiliza muziki, kuwasikia marafiki zake, walimu wake, mama yake na hata mdogo wake wa kiume anasema,  “Hii inanifurahisha. Ndoto zangu ni kuwa Waziri. Waziri Mkuu.”

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
1'47"
Photo Credit
UNICEF Rwanda