Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msafara wa vyakula Gaza washambuliwa, wapalestina 234 wauawa mwishoni mwa wiki

Msafara wa vyakula Gaza washambuliwa, wapalestina 234 wauawa mwishoni mwa wiki

Pakua

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotoa misaada ya kiutu huko Gaza, Mashariki ya Kati, yameripoti kuwa  kuwa msafara wa malori yaliyokuwa yamebeba vyakula umeshambuliwa kwa kombora leo baada ya mwisho wa wiki uliogubikwa na uhasama na mapigano yaliyosababisha kuuawa kwa wapalestina 234, na hivyo kuzidisha mvutano zaidi kwenye ukanda huo.

Ripoti za kushambuliwa kwa msafara huo zimetolewa na Tom White, Mkurugenzi wa Masuala katika Shirik ala Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA huko Gaza, ambaye kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, ameambatanisha picha mbili, zikionesha jinsi tela la lori lililosheheni vyakula likiwa limeshambuliwa na kitambaa cha hema kilichotumika kulifunika tela hilo kikiwa kimeraruka.

Amesema lori hilo lenye tela lilikuwa linasubiri kuingia Kaskazini mwa Gaza lilipopigwa kwa kombora la Israel kutoka majini.

“Tunashukuru hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa,” amesema Bwana White.

Kwenye picha hizo, maboksi kadhaa yenye misaada yameonekana kusambaa barabarani, lakini haikufahamika haraka kilichomo kwenye maboksi hayo.

Harakati za UNRWA kufikia eneo la kaskazini mwa Gaza zimekuja baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula, WFP kuripoti Ijumaa ya kwamba kwa mara ya tatu limeshindwa kufika kaskazini mwa Gaza.

Mkurugenzi wa WFP eneo la Palestina Matthew Hollingworth amesema waliweza kufikisha misafara minne tu mwezi Januari, sawa na malori 35 yenye shehena kwa ajili ya watu 130,000.

Afisa huyo wa WFP anasema chakula hicho hakitoshelezi kuepusha baa la njaa Gaza, kwani kiwango cha njaa kinazidi kuongezeka Gaza.

Ametumia ukurasa wake kwenye mtandao wa X kuonesha jinsi ilivyo vigumu kwa misafara ya misaada kuingia na kupita eneo lililozingirwa la Gaza baada ya takribani miezi minne ya mashambulizi yasiyokoma kutoka Israel.

Anasema, “kuna uharibifu kila mahali, vifusi, Barabara zimefungwa na vile vile kuna mapigano yanaendelea kwenye maeneo kadhaa ya ukanda huu. Inachukua muda kuratibu, kupita kwenye vizuizi.”

Audio Credit
Assumpta Massoi
Audio Duration
2'4"
Photo Credit
© UNICEF/Eyad El Baba