Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN: Raia 25, 000 wamepoteza maisha katika vita Gaza na mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka

UN: Raia 25, 000 wamepoteza maisha katika vita Gaza na mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka

Pakua

Mashambulizi makubwa ya mabomu yanayofanywa na Israel Gaza yameendelea tena leo sanjari na maroketi yanayovurumushwa na makundi yenye silaha ya Kipalestina kuelekea Israel, wakati wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wakiripoti kuuawa kwa watu zaidi ya 25,000 Gaza tangu kuanza kwa machafuko hayo mapya Oktoba 7 mwaka jana na mahitaji ya kibinadamu yakiongezeka kila uchao. 

Hali inazidi kubwa mbaya na hakuna dalili ya kukomesha uhasama Gaza limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA

Likinukuu takwimu za wizara ya afya ya Gaza mbali ya watu waliopoteza maisha Wapalestina zaidi ya elfu 62 wamejeruhiwa, wakati serikali ya Israel kwa upande wake ikisema tangu mwishoni mwa wiki askari wake wawili wameuawa na kufanya jumla ya askari wa Israel waliopoteza Maisha tangu kuanza kwa operesheni ya vita vya ardhini kufikia 193 na majeruhi zaidi ya 1200.

Leo mawaziri wa mambo ya nje wa Israel na Palestina wanajiandaa kukutana na wenzao wa Ulaya kwenye mazungumzo ya faragha mjini Brussels Ubeligiji, na hatua hii imekuja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa G-77 na China uliofanyika Kampala Uganda kulaani vikali umwagaji damu unaoendelea Gaza akisema ni unasikitisha na haukubaliki akisisitiza kufanyika kila linalowezekana kuzuia mgogoro huo kusambaa zaidi kikanda.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana na yanaongezeka kila siku, hivi sasa ni maduka 15 pekee ya kuoka mikate ndio yanayofanya kazi sita Rafah na tisa Deir al Balah na hakuna hata moja Kaskazini mwa Wadi Gaza.

Nalo shirika la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema kuendelea kutokuwepo kwa mawasiliano kwa siku ya saba sasa kunavuruga usambazaji wa misaada na watu kupata huduma muhimu zikiwemo za matibabu hasa ukizingatia kwamba watu milioni 1.7 wametawanywa na miongoni mwa raia waliouawa 335 walikuwa katika makazi ya UNRWA na wafanyakazi wa shirika hilo waliopoteza Maisha hadi sasa ni 151.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'22"
Photo Credit
© UNICEF/Eyad El Baba