Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi wa jimboni Anambra, Nigeria wapata bima ya afya kwa bei nafuu kwa usaidizi wa WHO

Wananchi wa jimboni Anambra, Nigeria wapata bima ya afya kwa bei nafuu kwa usaidizi wa WHO

Pakua

Nchini Nigeria katika Jimbo la Anambra shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kanda ya Afrika kwakushirikiana na mpango wa Bima ya Afya ya Serikali wanabadilisha maisha ya wananchi kwa kulipia sehemu kubwa ya gharama za matibabu ili kuhakikisha kila mtu anaweza kupata huduma za afya bila kudumbukia katika umaskini. 

Anambra ni jimbo la nane lenye wakazi wengi nchini Nigeria na jimbo la pili kwa idadi kubwa ya watu baada ya jimbo la Lagos. Wananchi wa jimbo hili wanachangamkia kujiandikisha katika mpango wa jimbo hilo wa bima ya afya ambapo WHO inatoa usaidizi kupitia mafunzo na miongozo ya kimkakati.

Zaidi ya wananchi 225,000 wameshakata bima ya afya na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Bima ya Afya la jimbo la Anambra Dokta. Simeon Onyemaechi anaeleza malengo yao.

“Hakuna mtu anayepaswa kuwa maskini kwa sababu anahitaji huduma ya afya. Tumewapa  wananchi ulinzi wa hatari za kifedha ili kuwaokoa kutokana na matumizi makubwa ya afya kwa njia ambayo hakuna hata mtu mmoja anayepaswa kukabiliwa na ugumu wa kifedha au kuwa maskini kwa sababu alilazimika kulipa bili kubwa za hospitali.”

Mpango huu unawashirikisha viongozi wa kimila, mmoja wao ni Mfalme Ben Emeka, wa himaya ya Umueri.

“Bima ya Afya ni jambo la ajabu ambalo limekuja jimbo la Anambra na limefika kwa watu wangu, watu wa Umueri, kwa sababu kabla ya sasa walikuwa wakilipa kiasi kikubwa sana.”

Sio tu Mfalme Emeka anahamasisha wananchi wake kukata bima za afya lakini pia amekatia wananchi wake 300 bima ya afya na anatoa wito kwa watu wenye uwezo wa kifedha na ushawishi kufanya kama yeye.

“Matajiri sasa wanaweza kuwasaidia masikini kwa kuwakatia bima za afya. Na masikini pia wanaweza kujilipia wenyewe bima za afya kwakuwa bei imekuwa nafuu.”

Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
2'9"
Photo Credit
OCHA/ Trond Jensen