Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi ufanywe Gaza kuhusu madai ya ukatili wa kingono wakati wa shambulio la Hamas - OHCHR

Uchunguzi ufanywe Gaza kuhusu madai ya ukatili wa kingono wakati wa shambulio la Hamas - OHCHR

Pakua

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk leo amelaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki wa kingono dhidi ya Waisraeli unaodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa Hamas wakati wa mashambulizi yao ya kigaidi kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, huku wahudumu wa kibinadamu huko Gaza wakionya kuhusu hali mbaya ya raia. 

Kamishina mkuu Türk akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis amesisitiza kuhusu hofu yake kwa hatma ya raia akirejea wito wa kukomesha uhasama mara moja kunusuru Maisha ya raia na miundombinu yao. 

Na kuhusu madai ya Umoja wa Mataifa kuwa na misimamo miwili kunapokuja masuala ya ukatili Gaza amekanusha madai hayo na kubainisha kuwa amefahamishwa kuhusu madai ya unyanyasaji wa kijinsia na kingono wakati wa shambulio la Hamas kwa jamii za kusini mwa Israeli.

Amesema kwa uchungu mkubwa kwamba “Ni bayana kwamba mashambulizi ya kikatili yanapaswa kuchunguzwa kikamilifu, kwa uchunguzi huru kwa sababu hilo ni deni letu kwa waathirika.”

Juliette Touma, ambaye ni msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA, wakati wa mahojiano na vyombo vya habari yaliyochapishwa mtandaoni leo kuhusu hali mbaya ya raia Gaza amesema "Nadhani tumegonga mwamba na ni hatua ya mabadiliko katika vita hivi  hali inazidi kuwa mbaya kila dakika tunapokea simu za mara kwa mara za dharura kutoka kwa wafanyakazi wenzetu na marafiki."

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA mapambano yameshika kasi Israel ikishambulia kila kona kwa njia ya anga, baharini na ardhinihususan Mashariki mwa mji wa Gaza kwenye na kuna tarifa za takribani watu 60,000 kuwasili katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia na Khan Younis saa chache zilizopita na Hamas inaendelea kuvurumisha maroketi kwenda Israel kutokea Gaza.

Mbali ya changamoto kubwa za kiafya kutokana na mrundikano wa watu na mazingira machafu sasa shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP WFP linaonya kuhusu janga kubwa la njaa.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
1'53"
Photo Credit
©UNICEF/UNI472270/Zaqout