Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kalavati 'lasogeza' huduma za afya kwa wanajamii Gambia

Kalavati 'lasogeza' huduma za afya kwa wanajamii Gambia

Pakua

Nchini Gambia, Magharibi mwa bara la Afrika, kalavati au daraja dogo lililojengwa na shirika la Umoja wa Mataifa la maendeleo ya mitaji, UNCDF kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU)ili kuunganisha maeneo mawili, Pakaliba na Baro Kunda, limesogeza huduma ya afya karibu na wakazi wa maeneo hayo. Anold Kayanda na maelezo zaidi

Gambia vijijini, Sarata Ceesay, ili kuhudhuria uchunguzi wa baada ya kujifungua hahitaji tena kupita kwenye maji ambako mamba hupenda kukusanyika. Pia halazimiki kulipa nauli kuzunguka kilomita nne kuikwepa adha ya kupita kwenye maji ambayo hujui utaliwa na mamba au utazama maji. Shukrani kwa ujenzi wa kalavati hili jipya.

Bi Ceesay, anaweza kujikinga dhidi ya hofu ya kifo cha mtoto mwingine, binti yake Awa ambaye pacha wake alishafariki akiwa kichanga kwa sababu ya changamoto hizi za huduma ya afya, “tulilazimika kuruka kutoka jiwe moja hadi jingine kuvuka mto.” Anasema.

Buba Jobe, Muuguzi na Mkunga wa Afya ya Jamii, Kituo cha Afya cha Pakaliba, Gambia anathibitisha mabadiliko haya chanya,

"Sasa kwa kuwa wanaweza kutembea kwa urahisi kutoka Baro Kunda hadi Pakaliba bila kulipa nauli yoyote, hiyo imefanya huduma ya afya kufikika. Wanaweza kuja wakati wowote. Kwa hivyo hiyo imeongeza mtiririko wa wagonjwa wetu katika idara ya wagonjwa wa nje.”

Audio Credit
Assumpta Massoi/Anold Kayanda
Audio Duration
1'30"
Photo Credit
UN News/ Hisae Kawamori