Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women: Mzozo wa Mashariki ya Kati ni jinamizi kwa wanawake na wasichana

UN Women: Mzozo wa Mashariki ya Kati ni jinamizi kwa wanawake na wasichana

Pakua

Mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati baina ya kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas na Israel kwa siku 18 sasa umesababisha jinamizi kubwa kwa maelfu ya wanawake na wasichana limesema shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya wanawake UN Women.

Milio ya makombora na risasi vimekuwa vikitawala Gaza, watu kwa maelfu wakipoteza maisha na wengine kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani. Akizungumza na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa Sarah Hendriks naibu mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women Sara Hendricks amesema miongoni mwa waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana na ni kutoka pande zote za mzozo.

Amesema  hali ni mbayá "Kwa kweli huu ni wakati wa giza na mgumu sana. Ni mzozo mkubwa tofauti na wowote ambao eneo hili limewahi kushuhudia katika miongo kadhaa. Tunasikitishwa sana na athari zake kwa maisha ya wanawake na wasichana. Ni wazi kwamba wengi sana tayari wamepoteza maisha au wapendwa wao.” 

Sara amesema ili kuepusha madhila zaidi kwa wasichana na wanawake hawa UN Women iko msatari wa mbele kuwasaidia kwa kila hali na pia “Wito wa UN women umekuwa ni kuhakikisha ulinzi kwa wanawake na wasichan Israel na eneo linalokaliwa la Palestina na kuhakikisha vita vinasitishwa mara moja kwa sababu za kibinadamu. Kuendelea kwa machafuko haya na athari zake kutaleta hatari za kijinsia kwa wanawake kwenye Ukanda wa Gaza.”

Amezitaja hatari hizo kuwa ni pamoja na idadi kubwa ya vifo, ongezeko la wajane, hofu ya ukatili wa kijinsia  na kaya nyingi kuendeshwa na wanawake pekee .

Sara amesema suluhu pekee ni Amani”Kinachohitajika ni usitishwaji haráka uhasama kwa minajili ya amasuala ya kinidamu, fursa ya bila vikwazo kuingiza misaada ya kibinadamu ikijumuisha mahitaji ya msingi kwa kila kaya, kwa kila maisha chakula, maji, vifaa vya nyumbani na hususani mafuta, ni muhimu kwa Maisha ya wanawake na wasichana kwenye Ukanda wa Gaza.”

Amesisitiza kuwa kinachowakabili wanawake na wasicha hawa lazima kiwe kitovu cha suluhu

“Ni muhimu sana kwa kipaumbele cha wanawake na wasichana wakati hali hii ikiendelea kieleweke vyema, na ndio sababu UN Women imetoa muhtasari unaotathimini haraka hali ya kijinsia katika mzozo wa sasa.”

Afisa huyo wa UN Women amesema kwa muda mrefu kumekuwa na wanawake wanaharakati Gaza ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kusaidia masuala ya kibinadamu kwa wanawake wenzao lakini sasa ukurasa umepinduliwa “Mambo yamebadilika kwa wanawake ambao walikuwa wanaharakati wa kuchagiza hatua za kibinadamu kwa misingi ya kijinsia kwani sasa wamejikuta ni walengwa wa hatua hizo za kibinadamu .” 

Licha ya changamoto zinazoendelea kwa wanawake hao wa Mashariki ya Kati Sarah ameahidi kwamba UN women haitowapa kisogo wanawake hao “Tutaendelea kusalia hapokusikiliza sauti za wanawake na wasichana, kusikiliza mtazamo wao na kuuwasilisha kwenye jumuiya ya kimataifa ili mahitaji yao yapewe kipaumbele hata wakati suluhu ya mzozo mzima ikiwa inashughulikiwa.”

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
3'35"
Photo Credit
© UNICEF/Hassan Islyeh