Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia katika ukanda wa Gaza hawana pa kukimbilia, milioni 1 waambiwa waondoke ndani ya saa 24: UN

Raia katika ukanda wa Gaza hawana pa kukimbilia, milioni 1 waambiwa waondoke ndani ya saa 24: UN

Pakua

Leo ni siku nyingine ambapo hali imeendelea kuwa tete na mbayá zaidi kwenye Ukanda wa Gaza, kwani Israel imetangaza watu wote wanaoishi katika eneo la Kaskazini mwa Wadi Gaza kuondoka na kwenda Kusini mwa Gaza ndani ya saa 24 na hivyo kuwaacha njiapanda maelfu kwa maelfu ya watu wanaoishi eneo hilo yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa hii leo ambayo yanahaha kuwasaidia na kuwanusuru watu hao. 

Umoja wa Mataifa umesema amri hiyo ya watu kuondona inawaathiri zaidi ya Wapalestina milioni moja wakiwemo watoto, wazee na wagonjwa ikiwalazimisha kuhamia kwingine wakati hawana chochote na hata usafiri, pia kukiwa na hakikisho dogo sana kwa ajili ya usalama wao wakati mashambulizi yakiendelea.

Umoja wa Mataifa unasema unadhani itakuwa vigumu sana kuendesha shughuli hiyo ya kuhama bila kuleta madhara makubwa ya kibinadamu, hivyo umeto ombi la kufuta amri hiyo ili kuepuka zahma kubwa zaidi katika hali ambayo tayari ni mbayá.

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametoa wito kwa mataifa yote kusisitiza na kuzisaidia pande kinzani katika mzozo kutekeleza utoaji mwanya wa fursa ya misaada ya kibinadamu ili kuhakikisha msaada unaohitajika haraka unawafikia wenye uhitaji.

Pia ameonya kwamba katika nchi nyingi hivi sasa kumekuwa na ongezeko la chuki dhidi ya Wayahudi na kauli za chuki dhidi ya Uislam amelaani vikali hayo.

Ndani ya Gaza kamisha mkuu wa shirika laumoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini amezitaka pande zote na wale wenye ushawishi juu ya pande hizo kukomesha madhila yanayoendelea na kuhakikisha msaada na ulinzi kwa raia wote.

Amesisitiza kwamba amri iliyotangazwa na Israel kutaka zaidi ya watu milioni moja kuondoka” Hii itasababisha janga kubwa ambalo halijawahi kushuhudiwa na kuwasukuma zaidi jehanamu watu wa Gaza.”

Ili kutoa msaada ipasavyo Umoja wa Mataifa unasema fedha zinahitajika ndio maana leo shirika lake la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA limezindua ombi la dola milioni 249 kwa ajili ya washirika wake wa kibinadamu 77 watakaokuwa wakihudumia mahitaji ya haraka ya watu milioni 1.26 Gaza na kwenye Ukingo wa Magharibi.

Na shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limeonya kuhusu vifo, majeruhi na machungu wanayopitia watoto wasio na hatia katika mzozo huu , huku lile la afya duniani WHO likisema mfumo wa afya Gaza hauana uwezo tena wa kutoa huduma zinazohitajika hasa kutokana na hospital nyingi kusambaratishwa na makombora na kutokuwa na vifaa vinavyohitajika.

Wito wa mashirika haya ni mmoja tu, mgogoro huu lazima ukome mara moja kunusuru maisha ya raia wa pande zote mbili. 

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
WHO/Occupied Palestinian Territory