Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Idadi ya watoto waliotawanywa duniani imevunja rekodi na kufikia milioni 43.3

UNICEF: Idadi ya watoto waliotawanywa duniani imevunja rekodi na kufikia milioni 43.3

Pakua

Katika kuelekea siku ya wakimbizi duniani itakayoadhimishwa wiki ijayo, ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imeonya kwamba idadi inayoongezeka ya watoto kutawanywa duniani, inadhihirisha jinsi gani dunia ilivyoshindwa kushughulikia mizizi ya watu kutawanywa na kutoa suluhu ya muda mrefu hususan kwa watoto wanaolazimika kukimbia makwao.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo mjini New York hadi kufikia mwisho wa mwaka jana 2022 makadirio ya UNICEF yanaonyesha kwamba watoto milioni 43.3 walilazimika kuishi maisha ya kutawanywa na wengi wao katika utoto wao wote.

Ripoti inasema idadi ya watoto waliofurushwa kwa lazima kutoka makwao iliongezeka maradufu katika muongo uliopita, na hivyo kupita juhudi za kuweza kuwajumuisha na kuwalinda wakimbizi na watoto ambao ni wakimbizi wa ndani. Na vita nchini Ukraine imechochea hali kuwa mbaya zaidi ikiwalazimu zaidi ya watoto milioni 2 wa Ukraine kuikimbia nchi hiyo na kkuwafanya wengine zaidi ya milioni 1 kuwa wakimbizi ndani.

Akizungumzia jinamizi hili mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema."Kwa zaidi ya muongo mmoja, idadi ya watoto wanaolazimika kuhama makwao imeongezeka kwa kasi ya kutisha, na uwezo wetu wa kimataifa wa kukabiliana na hali hiyo bado uko katika shinikizo kubwa. Ongezeko hilo linakwenda sambamba na mashambulizi ya mara kwa mara ya migogoro, changamoto na majanga ya tabianchi duniani kote. Lakini pia inadhihirisha hali duni za serikali katika kuhakikisha kila mkimbizi na mtoto aliyetawanywa ndani ya nchi anaweza kuendelea kusoma, kuwa na afya njema na kuendelea ili kufikia uwezo wake kamili.”

Miongoni mwa watoto hai milioni 43.3 waliolazimika kutawanywa takribani asilimia 60 sawa na watoto milioni 25.8 walikuwa ni wakimbizi wa ndani waliotokana na mizozo na machafuko.

Na idadi ya watoto wakimbizi na wasaka hifadhi ilifikia kiwango cha juu cha watoto milioni 17.5 bila kujumuisha watoto waliotawanywa mwaka huu wa 2023.

Kwa mantiki hiyo UNICEF imetoa wito kwa serikali zote kutomwacha mtoto yeyote nyuma kwa kutambua watoto wakimbizi, wahamiaji na waliotawanywa cha kwanza ni watoto na wana haki ya kulindwa, kujumuishwa na kushirikishwa. 

Pili imezitaka serikali kutoa njia salama na za kisheria kwa watoto kuweza kuhama, kuomba hifadhi na kujumuishwa na familia zao.

Tatu kuhakikisha hakuna mtoto anayeshikiliwa kwa sababu ya hali yake ya uhamiaji au kurejeshwa bila mazingira salama isipokuwa tu pale ambapo imebainika kuwa ni kwa maslahi ya mtoto.

Nne imezitaka serikali kuimarisha mifumo ya kitaifa ya elimu, afya, ulinzi kwa watoto na mifumo ya hifadhi ya jamii ili kujumuisha watoto waliotawanywa bila ubaguzi.

Tano kuwekeza katika mifumo ya ulinzi kwa watoto ili kuweza kuwalinda vyema watoto walio safarini dhidi ya hatari za kunyanyaswa na ukatili hususan watoto wanaokimbia peke yao bila walezi au wazazi.

Na mwisho imezitaka serikali kusikiliza na kuwahusisha watoto katika kusaka suluhu ambazo ni endelevu na jumuishi na ambazo zinaweza kuwasaidia watoto hao kufikia uwezo wao.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
3'22"
Photo Credit
UN News/Byobe Malenga