Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Sudan sitisheni mzozo hali ya watoto inazidi kuwa mbaya

UNICEF: Sudan sitisheni mzozo hali ya watoto inazidi kuwa mbaya

Pakua

Msikilizaji, Usemi ambao umekuwa ukielezwa mara zote watu wanapozungumzia suala la amani ni kwamba, vita inapotokea wanaotesema ni wanawake na watoto. Kwa zaidi ya wiki moja nchi ya Sudan imekuwa katika vita ya madaraka baina ya majeshi ya nchi hiyo. Je hali ya watoto ipoje?

Hata kabla ya kuanza kwa mzozo wa hivi karibuni nchini Sudan, mahitaji ya kibinadamu kwa watoto yalikuwa juu sana. Takwimu zikionesha robo tatu ya watoto walikadiriwa kuishi katika umaskini uliokithiri, na watoto milioni 11.5 na wanajamii walihitaji huduma za dharura za maji na usafi wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Geneva Uswisi msemaji wa Shirika la moja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF James Elder anaeleza hali ilivyo sasa.

“Kwasasa tuna ripoti zinazoonesha angalau watoto 9 waliuawa na wengine 50 wamejeruhiwa. Idadi hiyo itaendelea kuongezeka maadamu mapigano yanaendelea. Lakini jambo la muhimu sana kukumbuka ni kwamba katika mapigano haya, idadi kubwa ya watu wamekwama hawawezi Kwenda kokote hivyo hawana huduma ya umeme, na wana wasiwasi wa kuishiwa chakula, maji na dawa.”

Watoto waliokuwa na utapiamlo mkali kabla ya vita kuanza, walikuwa wamelazwa hospitalini hali ikoje huko?

“Hivi sasa tupo katika hali ambayo misaada muhimu ya kuokoa maisha kwa zaidi ya watoto 50,000 iko hatarini, hawa ni watoto wenye utapiamlo mkali. Kwasasa watoto hawa wapo mahospitalini kwa sababu wanahali mbaya zaidi, kwa hiyo wanalishwa kwa mirija kwa sababu hiyo ndiyo njia pekee ya kulishwa, na wakati mashambulizi ya mabomu au makombora yanapoanza nje ya hospitali, watoa huduma za matibabu wanahitaji kukimbia kujificha. Halafu nini sasa kinaendelea?”

Ama hakika suluhu ya haraka inahitajika ili si tu kukomesha vita bali pia kuokoa maisha ya watoto hawa na wanajamii kwa ujumla ikiwemo wafanyakazi wa misaada yakibinadamu.

Tangu kuibuka kwa mapigano, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekuwa akisema, inahitajika nguvu ya pamoja kukomesha mara moja uhasama, na pande zote zinazo zozana zinahitajika kuheshimu majukumu yao ya kimataifa ya kuwaweka watoto mbali na madhara. Na msemaji wa UNICEF anarejea wito huo wa Guterres akieleza nini kifanyike.

“Nini sasa kifanyike, kwasasa ni kuendelea kukazia wito wa Katibu Mkuu kwamba inahitajika kusitishwa kwa mapigano kwa sababu mapigano yamekuwa ya kiholela na watumishi wengi na wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayotegemewa na wengi kwa sasa wamejificha, na wengine wamekwenda kwenye Mto Nile kujaribu kupata maji licha ya ukosefu wa usalama, iwe kupata maji safi na usafi wa mazingira au kupigwa na silaha za moto.”

Audio Credit
Leah Mushi
Sauti
2'54"
Photo Credit
© UNICEF/Mojtba Moawia Moawi