Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD limesema mwaka 2022 umekuwa mgumu ukiziacha familia nyingi zikihaha kuweka mlo mezani

UNCTAD limesema mwaka 2022 umekuwa mgumu ukiziacha familia nyingi zikihaha kuweka mlo mezani

Pakua

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo UNCTAD imesema mwaka huu wa 2022 umekuwa mgumu sana ambapo familia nyingi zimekuwa zikihaha kuweka mlo mezani na kujikimu hadi mwisho wa mwezi, lakini kuna suluhu na suluhu hizo zinapaswa kuwa za kimkakati na za kimataifa.

Kauli hiyo ni kwa mujibu wa Rebeca Grynspan katibu mkuu wa UNCTAD akihojiwa katika kipindi maalum cha UNCTAD Tradecast kuhusu kumalizika mwaka huu wa 2022 na kinachotarajiwa mwakani. 

Bi. Grynspan amesema Hali ngumu mwaka huu imechangiwa na athari za kiuchumi zilizotokana na janga la COVID-19 na kujikwamua kwa polepole kutoka kwenye janga hilo, athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mafuriko, lakini pia vita ya Ukraine imesababisha gharama kubwa ya maisha kupanda kote duniani, kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kuendelea kupanda kwa kiwango cha riba na nchi nyingi zinazoendelea kukabiliwa na mzigo usiobebeka wa madeni.” 

Ameongeza kuwa ingawa nchi zilizoathirika zaidi ni zinazoendelea lakini nchi zilizoendelea pia zimepata changamoto lakini tofauti ni kwamba zina nyenzo za kukabiliana na changamoto hizo zaidi ya mataifa duni. 

Katibu mkuu huyo wa UNCTAD amesisitiza kuwa kuna suluhu “Kuanzia katika kiwango cha kitaifa kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa kisera, hatua za kulinda watu lakini mwisho wa siku suluhu zinategemea hatua zilizoratibiwa za jumuiya ya kimataifa  na ndicho tunachojaribu kukisukuma mbele.” 

Pamoja na hatua hizo amesema pengo la usawa linazidisha changamoto hivyo kuliziba kutaongeza mnepo kwa dunia kupambana na changamoto hizi. 

Na kuhusu matarajio yake kwa mwaka ujao amesema “Natumai kwa dunia kutambua wajibu tulionao sasa, tunahitaji uratibu, mshikamano, hatua za pamoja na dunia iliyoungana ambayo inahitaji ujarisi na uongozi imara, natumai kuliona hilo 2023.” 

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'7"
Photo Credit
© WFP/Gabrielle Menezes