Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yawezesha wanafunzi waliokuwa karantini Uganda kufanya mitihani

UNICEF yawezesha wanafunzi waliokuwa karantini Uganda kufanya mitihani

Pakua

Nchini Uganda shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limewezesha wanafunzi wa shule moja ya msingi nchini humo kufanya mtihani wa kuhitimu shule ya msingi baada ya shule hiyo kulazimika kufungwa na wanafunzi kuwekwa karantini kufuatia mwanafunzi mmoja kupata maambukizi ya Ebola, mlipuko uliotangazwa mwezi SEptemba mwaka huu.

Tarehe 20 mwezi Septemba mwaka huu wa 2022, Wizara  ya Afya nchini Uganda ilitangaza mlipuko wa Ebola, mlipuko ambao ulihatarisha kuvuruga mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi kwa wanafunzi wa darasa la saba. 

Shule ya msingi ya Green Valley kwenye mji mkuu Kampala ilikuwa hatarini zaidi kwa sababu mwanafunzi mmoja aliambukizwa Ebola hivyo  madarasa matatu yalifungwa na shule ikafungwa ili ifanyiwe usafi. 

Mpaka Katula ni Mkurugenzi wa Shule ya msingi Ya Green Valley. “Uhai wa walimu wangu, wanafunzi wangu na wangu mwenyewe ulikuwa hatarini, ningaliweza kuachia shule, kwa hiyo kufunga shule lilikuwa ni jambo dogo.” 

Shule hiyo ilifungwa wiki tatu kabla ya kufanyika kwa mtihani ambapo Ian Mugisha mmliki wa shule ya msingi Green Valley anafafanua kwamba.. Hii mitihani hufanyika katika siku maalum iliyopangwa. Usipofanya siku hizo, hutaweza kufanya tena, lazima usubiri mwaka unaofuatia. Kwa maajabu Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Bodi ya Taifa ya mitihani Uganda, walishirikiana kuona wanafunzi wanafanya mitihani na UNICEF ikasaidia.” 

Jane, jina lake hili si rasmi ni mmoja wa wanafunzi 30 waliokuwa karantini na anasema, « UNICEF imenisaidia vifaa vya kufanyia mtihani, mlo wa mchana na usafiri kutoka nyumbani hadi hapa. Nilifanya mitihani ya kuhitimu darasa la Saba nikiwa karantini na nina imani nimefanya vizuri.” 

Na Bwana Katula anarejea na shukrani akisema, “sijui hii shule ingalifanya bila UNICEF kuingilia kati. Lakini kile ninachoweza kusema, asante UNICEF.” 

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
2'6"
Photo Credit
© UNICEF/Uganda