Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tubaki nyumbani au tuhame nchi? Wananchi Tunisia katika njiapanda!

Tubaki nyumbani au tuhame nchi? Wananchi Tunisia katika njiapanda!

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM limesema wananchi wengi wa Tunisia hivi sasa wanakabiliwa na machaguo magumu ya kubaki ndani ya nchi yao na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha na uhaba wa chakula au kukimbia nje ya nchi yao na kutojua nini kitatokea huko waendako. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi.

Katika soko la Kairouan nchini Tunisia mwanamke anaonekana akiwa sokoni akinunua nyanya na anasema….. "Naweza kusema nini? Bei zinapanda! Watu maskini hawawezi tena kumudu chochote. Ni kama dunia inawaka moto.”

Mwingine naye anasema... “Hakuna sukari, inamaana nilazima nichukue teksi ini niende mbali sana kununua kilo moja ya sukari."

Wakati wananchi wakilalamikia bei juu na kukosa bidhaa, wamiliki wa maduka ya jumla nao wanasema nao hawana bidhaa za kutosha kwa ajili ya wateja wao.

Samia Zwabi ni mmiliki wa duka la vyakula na anasema .... “Hatuwezi kufanya kazi. Tunafanya kazi kwa nusu ya uwezo wetu. Mteja anapokuja, hawezi kupata mahitaji yote ya msingi. Wateja wanaomba kitu ambacho sina. Sio kwa uchaguzi wetu hata sisi tunahitaji kuwa na uwezo wa kufanya kazi ili kuweza kulisha watoto wetu.”

Wananchi wengi wa Tunisia kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa vyakula muhimu, mafuta na bidhaa muhimu za kilimo  na hii yote unaelezwa kusababishwa zaidi na vita nchini Ukraine. Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji Safa Msehli anasema kwa sasa majaribu yamewafika shingoni wananchi na wengine wameamua kukimbia.

“Nadhani kile ambacho mzozo wa Ukraine umeibua tena, ni maamuzi magumu ambayo watu wanapaswa kufanya kila siku, kwa sababu watu wanaolazimika kukimbia makazi yao, watu wanaolazimika kukimbia nchi yao, hawachukui uamuzi huo kirahisi.”

Kupitia Mpango wa Nafaka wa Bahari Nyeusi Umoja wa Mataifa umekuwa ukijitahidi kufikisha mahitaji ya chakula kwenye maeneo ya uhitaji zaidi, na miezi miwili tu baada ya kuanza kwake zaidi ya tani 85,000 za ngano kutoka Ukraine zimewasili katika bandari za Tunisia.

Kiujumla wananchi wengi katika nchi mbalimbali wanakabiliwa na changamoto kama za Tunisia kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa, mafuta na huku changamoto nyingine za mabadiliko ya tabianchi zikififisha kabisa uwezo wao wa kujikimu hata kwa kilimo.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
2'31"
Photo Credit
UN News/Daniel Johnson