Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukraine na Urusi zatia saini makubaliano ya kuruhusu usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia bahari nyeusi

Ukraine na Urusi zatia saini makubaliano ya kuruhusu usafirishaji nafaka za Ukraine kupitia bahari nyeusi

Pakua

Hatimaye makubaliano ya kuruhusu meli zilizojaa shehena za nafaka kutoka nchini Ukraine zipite kwenye baharí nyeusi yamefikiwa hii leo huko Instanbul Uturuki baina ya Ukraine na Urusi yakishuhudiwa na katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye amesema makubaliano hayo yameleta nuru kwa ulimwengu kupata ahueni kwenye be iza mazao ya chakula katika soko la kimataifa.

Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi

 Makubaliano haya ni nuru,nuru ya matumaini, nuru ya unafuu ambao ulimwengu unahitaji kuliko zaidi hivi sasa kuliko hapo awali. Napenda kuwatambua na kuwashukuru wote waliohusika mpaka kufanikisha hatua hii.

Ndivyo alivyoanza hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huko Instanbul Uturuki baada ya kushuhudia utiaji saini baina ya Ukraine na Urusi kuruhusu meli zenye shehena ya mazao na nafaka zilizokuwa zimekwama katika mandari za Odessa, Chernomorsk na Yuzhny huko bahari nyeusi upande wa Ukraine.

Guterres amesema bila shaka haya ni makubaliano ya ulimwengu

“Yataleta ahueni kwa nchi zinazoendelea ambazo zipo kwenye makali ya kufilisika na watu walio hatarini zaidi wanaokabiliwa na njaa Kali.  Na yatasaidia kuleta utulivu wa bei za vyakula duiani ambazo tayari zilikuwa katika viwango vya rekodi mbaya hata kabla ya vita. Hili lilikuwa jinamizi la kweli kwa nchi zinazoendelea.”

Mbali na kuzishukuru nchi hizo mbili, Guterres amemshukuru Rais wa Uturuki Recep Erdogan kwa kuwa mwenyeji wa makubaliano hayo ambaye pia nchi yake itakuwa na jukumu muhimu la kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kufanya ukaguzi wa meli hizo za Ukraine ili zisibebe silaha za magendo wakati wa usafirishaji wa nafaka kwenda na zinaporejea kutoka katika soko la kimataifa.

Mashirika mengine ya UN yaliyohusika na mchakato huo ni lile la Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya kibinadamu OCHA na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kibiashara na maendeleo UNCTAD.

“Nipo hapa kuweka ahadi kamili kuwa Umoja wa Mataifa tutabakia kuwa wahusika wa karibu katika kufanyia kazi na kuhakikisha kuna mafanikio ya makubaliano haya. Tutaendelea kuongeza juhudi ili kuhakikisha UN iko katika nafasi nzuri ya kutekeleza ahadi zake. Ninavishukuru vikosi kazi vyote viwili vya Umoja wa Mataifa ambavyo vimetengeneza mkataba huu sawia, kwa uratibu thabiti.”

Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametangaza kikosi kazi cha kuwezesha utekelezaji wa mpango wa baharí nyeusi kikiongozwa ma Katibu Mkuu wa UNCTAD Rebecca Grynspan kikijikita katika kuwezesha upatikanaji usiozuiliwa wa chakula na mbolea zinazotoka nchini Urusi kwenda kwenye soko la kimataifa ikiwa pia ni utekelezaji wa moja ya vifungu vya makubaliano wa mkataba huo uliosainiwa hii leo.

“Nawaomba pande zote zisiache kipengele chochote na juhudi zozote za utelekezaji wa ahadi zao. Hatupaswi pia kuacha juhudi zozote kwa ajili ya amani, haya ni makubaliano ambayo hayajawahi kutokea kati ya pande mbili zinazohusika katika mzozo wa umwagaji damu”

Katibu Mkuu Guterres alihitimisha hotuba yake kwakusema nuru ya matumaini imeng’aa katika baharí nyeusi ni matokeo chanya ya kuhudi za pamoja za washirika wengi na kuhimiza katika nyakati za misukosuko ya dunia, nuru hii itaangaza njia ya kuelekea katika kupunguza mateso yanayowasibu wanadamu na kupatikana kwa amani.

Audio Credit
Assumpta Massoi/Leah Mushi
Audio Duration
3'19"
Photo Credit
Umoja wa Mataifa