Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

12 Mei 2022

12 Mei 2022

Pakua
Jaridani Alhamisi Mei 12, 2022 na Grace Kaneiya HABARI KWA UFUPI Mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masauala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths yuko ziarani nchi Kenya kwa lengo la kuitanabaisha jumuiya ya kimataifa janga la kibinadamu lililosababishwa na mabadiliko ya tabianchi katika Pembe ya Afrika, nchini Ethiopia, Somalia na Kenya. Zaidi ya watu milioni 15 hawana uhakika wa chakula kutokana na ukame mkali ambapo Kenya pekee watu milioni 3.5 wanakabiliwa na njaa huku viwango vya utapiamlo vikiongezeka mara mbili. Mwandishi wetu wa Kenya Thelma Mwadzaya amekuwa shuhuda wetu katika ziara hiyo iliyoanzia Lodwar jimbo la Turkana (TAARIFA YA THELMA) ===================== Wagonjwa wa COVID-19 wanaongezeka kwa wiki ya tatu mfululizo Kusini mwa Afrika wakati huu msimu wa baridi unapokaribia kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO. Shirika hilo linasema wagonjwa 46, 271 wamerekodiwa katika wiki iliyoishia tarehe 8 Mei 2022, ikiashiria ongezeko la asilimia 32% zaidi ya wiki iliyotangulia. Ongezeko hilo limechangiwa zaidi na idadi kubwa ya wagonjwa nchini Afrika Kusini ambapo visa vinavyorekodiwa kila wiki vimeongezeka mara nne katika wiki tatu zilizopita ingawa idadi ya vifo haijaongezeka sana. ================================ Na ikiwa leo ulimwengu unaadhimishwa kwa mara ya kwanza Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea, IDPH, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, limesema mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu zinabadilisha mifumo ikolojia na kuharibu bayonuai huku hali hiyo ikiunda maeneo mapya kwa ajili ya wadudu waharibifu kustawi. Aidha FAO imeeleza kuwa usafiri wa kimataifa na biashara, ambavyo vimeongezeka mara tatu katika muongo uliopita vimechangia kueneza wadudu na magonjwa. Umoja wa Mataifa uliipitisha tarehe 12 Mei kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Afya ya Mimea ili kuongeza uelewa wa kimataifa kuhusu jinsi kulinda afya ya mimea kunaweza kusaidia kutokomeza njaa, kupunguza umaskini, kulinda viumbe hai na mazingira na kukuza maendeleo ya kiuchumi na hivyo wito unatolewa kuchukua hatua za kuilinda mimea. MWISHO WA HABARI KWA UFUPI Katika mada kwa kina tunaangazia msanii wa uchoraji kutoka Tanzania. Kataika kujifunza neno la wiki linafafanuliwa neno mteremezi
Audio Credit
Grace Kaneiya
Audio Duration
12'37"