Lazima tutokomeze ukeketaji : Mwanaharakati Ifra Ahmed

Lazima tutokomeze ukeketaji : Mwanaharakati Ifra Ahmed

Pakua

Kutana na mkimbizi kutoka Somalia, muathirika wa ukeketaji ambaye hakuacha athari za jinamizi hilo kusambaratisha ndoto zake za kuhakikisha hatopumzika hadi pale mangariba wote watakapobwaga manyanga na kuacha ukatili huo nchini Somalia na kwingineko duniani. Kulikoni Flora Nducha anasimulia zaidi 

(TAARIFA YA FLORA NDUCHA) 
  Jina langu ni Ifrah Ahmed

Dublin nchini Ireland maskani  ya kudumu ya Ifra mkimbizi wa zamani aliyegeuka kuwa mwanaharakati wa kupinga ukeketaji na sasa anajivunia kuwa raia wa taifa hilo la barani Ulaya. 

Alizaliwa Somalia na ni muathirika wa ukeketaji. Vita viliposhika kasi mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 17 alifungasha virago na kuikimbia nchi yake , alifanikiwa pia kuwatoroka wasafirishaji haramu wa binadamu na hatimaye kupatiwa hifadhi nchini Ireland ambako 2010 alianza kampeni ya kutokomeza ukeketaji au FMG. 
 
Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Ifra anasema kwa nini aliamua kulivalianjuga suala hilo 
  (SAUTI YA IFRA CUT 1-MELLISSA) 
 
“Nilichotaka ni kuleta mabadiliko, kwa sababu sote tunajua kuwa FGM inasababisha vifo, matatizo ya figo na pia inasababisha athari nyingi za kiafya. Ni muhimu sana sio tu kwa Somalia bali kwa wanawake na wasichana duniani kote katika nchi ambako ukeketaji unafanyika  na pia kwa wasichana ambao wamezaliwa katika miji ya Ulaya ikiwemo hapa nchini Ireland kulindwa dhidi ya jinamizi hili.” 
Ifra ambaye tangu aingie Ireland aliapa kutopumzika hadi pale mangariba wote watakapozika visu na nyembe zao, juhudi zake kupitia Ifra Foundation zilianza kuzaa matunda baada ya bunge la Ireland kupitisha sheria kupiga marufuku ukeketaji na Joe Costello miongoni mwa wanasiasa mashuhuri wakati huo hakusita kuutambua mchango wake  
 (SAUTI YA JOE COSTELLO) 
“Nataka kuwapongeza baadhi ya watu walioonyesha ujasiri mkubwa na ambao wamekuwa msitari wa mbele katika suala hili, lakini hakuna mtu ambaye amefanya kazi zaidi kama msichana anayeitwa Ifra Ahmed.” 
 
Ifrah ni muungaji mkono mkubwa  wa UNHCR kwani yeye mwenyewe alikuwa mkimbizi lakini mchango wake ulichukua sura mpya mwaka jana 2020 alipoweka bayana kwamba amejitolea maisha yake  kusaidia kutokomeza Ukeketaji  na kutoa msaada wa ujumuishwaji kwa wahamiaji na wakimbizi vijana kutoka Afrika wanaoingia Ireland. 

Hivi sasa ana mtoto mmoja wa kike na amesema atahakikisha anamlinda dhidi ya shubiri aliyoionja 
(SAUTI YA IFRA 2-MELLISSA) 
“Mungu amenipa zawadi, binti yangu amezaliwa hapa Ireland na kamwe hatoonja machungu niliyopitia, hatopata athari zilizopata mimi. Na kuwa naye kunanifanya niwe na nguvu zaidi na sababu ya kuendelea kupambana.” 
TAGS: UNHCR, Ireland, Dublin. Ifra Ahmend, Ukeketaji, FGM 
 

Audio Credit
Leah Mushi/Flora Nducha
Audio Duration
2'49"
Photo Credit
UNICEF/Henry Bongyereirwe