Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nchi za Afrika ziko mbioni kuwa na soko moja la biashara:FAO/AU

Nchi za Afrika ziko mbioni kuwa na soko moja la biashara:FAO/AU

Pakua

Hii leo mjini Accra, Ghana, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO na Idara ya Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Bahari na Maendeleo Endelevu ya Muungano wa Afrika, AUC-DARBE, wamezindua mwongozo wa kukuza biashara ya kilimo miongoni mwa mataifa ya Afrika chini ya makubaliano mapya ya Eneo la Biashara Huru barani humo,  AfCFTA. Anold Kayanda na taarifa zaidi

(TAARIFA YA ANOLD KAYANDA)

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na FAO na AU, Mfumo wa Kukuza Biashara baina ya Afrika katika Bidhaa na Huduma za Kilimo ni mwongozo wa kupanua biashara ya kilimo miongoni mwa nchi za Kiafrika na unakusudia kufungua uwezo wa sekta ya kilimo kuchangia ukuaji endelevu na unaojumuisha.  

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa FAO ambaye pia ni Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Abebe Haile-Gabriel, Kamishna wa Muungano wa Afrika, Josefa Sacko, na Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene kwa pamoja katika utangulizi wa chapisho la mwongozo, wamesema, "mfumo huo unatoa kichocheo cha wakati unaofaa kwa mabadiliko bora zaidi, mifumo shirikishi ya kilimo-chakula, inayojumuisha, thabiti na endelevu, maendeleo endelevu na ustawi barani Afrika. Kipaumbele muhimu ni kufuata sera na mipango ya mabadiliko ya viwanda ambayo inasaidia sekta binafsi kuongeza thamani kwa bidhaa za kiafrika zinazokwenda nje, kushindana na uagizaji kutoka nje ya Afrika na kupanua fursa za kuzalisha kazi." 

Taarifa pia imeeleza kuwa Afrika ni eneo linaloagiza bidhaa za kilimo na chakula kutoka nje zenye thamani yad ola bilioni 80 kila mwaka, kama vile nafaka, nyama, bidhaa za maziwa, mafuta na sukari. Ni sehemu ndogo ya jumla ya biashara ya kilimo barani Afrika iko  miongini mwa nchi nyingine za Kiafrika. Biashara ya kilimo ndani ya Afrika inakadiriwa kuwa chini ya asilimia 20.

Kubadilisha ahadi kuwa vitendo 

Mfumo au mwongozo huo utasaidia watunga sera na sekta binafsi kuandaa mikakati, sera na mipango ya kukuza biashara ya kilimo baina ya nchi za Afrika na ukuzaji wa minyororo ya thamani ya kilimo, ili wadau, wakiwemo wakulima, wafanyabiashara wadogo na wa kati wa kilimo, wanawake na vijana, waweze kupata faida ya soko moja la AfCFTA. Maeneo ya utekelezaji ni pamoja na sera ya biashara, uwezeshaji wa biashara, uwezo wa uzalishaji, miundombinu inayohusiana na biashara, fedha za biashara, ujumuishaji wa soko na masuala mtambuka ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mifumo ya habari ya biashara na soko. 

Nchi za Kiafrika zimeweka ahadi za kuondoa ushuru kwa asilimia 90 katika zaidi ya msururu wa ushuru zaidi ya 5,000. Inakadiriwa kuwa ushuru huria katika awamu ya mpito kunaweza kuleta faida ya ustawi wa hadi Dola za Kimarekani bilioni 16.1, na ukuaji katika biashara ya jumla ya ndani ya Afrika kufikia asilimia 33, kutoka asilimia 15. 

Eneo la soko huru barani Afrika, AfCFTA linakuja baada ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kufikia makubaliano mnamo 2014 kufanya biashara mara tatu zaidi miongoni mwa mataifa ya Afrika katika bidhaa na huduma za kilimo ifikapo mwaka 2025 kama sehemu ya Azimio la Malabo. 

Biashara katika eneo la soko huru barani Afrika, AfCFTA limeanza biashara mnamo Januari mosi mwaka huu wa 2021 na ndio eneo kubwa zaidi la biashara huria ulimwenguni kulingana na idadi ya nchi zilizomo. AfCFTA inawakilisha soko la watumiaji bilioni 1.2. 

Audio Credit
UN News/ Anold Kayanda
Audio Duration
3'28"
Photo Credit
© FAO-Magnum Photos/Alex Webb