Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR mkombozi wa wakimbizi wajawazito wa Eritrea walioko Libya.

UNHCR mkombozi wa wakimbizi wajawazito wa Eritrea walioko Libya.

Pakua

Kama sehemu ya huduma mbali mbali za ulinzi zinazotolewa kwa wakimbizi na wanaotafuta hifadhi nchini Libya, shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR kupitia mdau wake, Kamati ya kimataifa ya uokozi, IRC, wanatoa huduma za afya ya uzazi bila malipo kwa wanawake ambao ni wajawazito au wamejifungua hivi karibuni, na pia kuwapatia rufaa za kwenda kwenye vituo vikubwa zaidi kwa ajili ya kujifungua. Ahimidiwe Olotu na maelezo zaidi.

Rahma ni mkimbizi kutoka Eritrea aliyeko ukimizini nchini Libya. Anaonekana akiwa ameambatana na mumewe na mtoto wao mchanga kuja katika kituo cha kuhudumia wanawake wajawazito na watoto kinachofadhiliwa na UNHCR na IRC. 

Mtoto Tarik ana umri wa siku 12. Yeye na mama yake wanapata uchunguzi wa kimatibabu. Hii ni mara ya kwanza kwa Rahma kujifungua la alikuwa na changamoto wakati wa kujifungua ambazo zilimlazimisha kufanyiwa upasuaji. Rahma anaeleza huduma za kituo hiki zilivyomsaidia, "Ujauzito ulikuwa mgumu. Daktari aliniona kwa uchunguzi wa kawaida na akanipa dawa. Alinisaidia. Wakati wowote nilipokuja hapa, daktari alikagua afya yangu na ya mtoto wangu, na sisi sote tuko sawa." 

Kwa wastani, zaidi ya wanawake 40 hufanyiwa uchunguzi wa mwenendo wa ujauzito katika kituo hicho kila mwezi. Huduma hii ni muhimu kwani ni vigumu na pia ni gharama kubwa kwa wakimbizi ambao hawana nyaraka rasmi za utambulisho kuweza kupata huduma katika vituo vya msingi vya afya nchini Libya. Darin Rafifi ni daktari wa magonjwa ya wanawake, anasema, "Wanawake wengi huja hapa kufuatilia masula ya ujauzito na magonjwa ya wanawake. Kwa sababu, wengi wao, hawana namna ya kuzifikia hospitali za umma, pengine kwa sababu ya masuala ya usalama na pia maeneo yako mbali sana nao." 

Mtoto Tarik ameandikiwa dawa. Mfamasia anaonekana akimkabidhi baba wa Tarik huku mama Tarik akiwa amembeba mtoto huyo na sasa wako tayari kurudi nyumbani kwa uhakika wa afya ya mtoto wao.  

 

Audio Credit
Grace Kaneiya/Ahimidiwe Olotu
Audio Duration
2'13"
Photo Credit
UNSMIL/Lason Athanasiadis