Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chanjo dhidi ya Ebola DRC yaanza kutolewa eneo ambalo mgonjwa wa kwanza alipatikana

Chanjo dhidi ya Ebola DRC yaanza kutolewa eneo ambalo mgonjwa wa kwanza alipatikana

Pakua

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limeanza kutoa chanjo dhidi ya Ebola kwa wakazi wa eneo la Butembo jimboni Kivu Kaskazini, ikiwa ni wiki moja baada ya mgonjwa mmoja kuthibitishwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
(Taarifa ya Assumpta Massoi)
Nats..
Eneo la Butembo katika hospitali ya Matanda, wahudumu wa afya wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi ya kujikinga dhidi ya Ebola, ikiwemo barakoa wakijandaa kutoa chanjo dhidi ya gonjwa hilo lililoripotiwa kuibuka tena kwenye jimbo hili la Kivu Kaskazini.
Chanjo zinapatiwa wale walio hatarini zaidi kuambukizwa Ebola na utoaji chanjo umeanzia hapa ukanda wa kiafya wa Biena katika hospitali ya Matanda ambako ndiko mgonjwa wa kwanza alipatiwa matibabu kabla ya kufariki dunia.
Watoa chanjo wakijiandaa, maafisa wa WHO nao wanapatiwa maelezo ikiwemo kwamba utoaji wa chanjo unafanyika pia katika ukanda wa afya wa Katwa mjini Butembo wakati huu ambapo tayari watu wanne wamethibitishwa kuwa na Ebola na wawili wamefariki dunia.
Kazi ya utoaji chanjo inaanza na WHO inasema takribani dozi 1200 za chanjo ziliwasilisha Butembo wiki iliyopita na dozi nyingine 1200 zimewasili Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
WHO ina uhakika kuwa DRC ina dozi za kutosha za chanjo dhidi ya Ebola kwa ajili ya kuchanja watu 16,000 wakiwemo wahudumu wa afya na walio hatarini kuambukizwa.
Wiki iliyopita, serikali ya DRC ilitoa taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola jimboni Kivu Kaskazini.
Eneo la Butembo ni eneo ambalo lilikuwa kitovu cha mlipuko wa 10 uliotangazwa kumalizika mwezi Juni mwaka jana.
 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta massoi
Audio Duration
3'19"
Photo Credit
WHO/Lindsay Mackenzie