Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa gereza kuu la Bunia, DR Congo, MONUSCO yaingilia kati.  

Njaa gereza kuu la Bunia, DR Congo, MONUSCO yaingilia kati.  

Pakua

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO umechukua hatua kukabiliana na njaa kwenye gereza kuu la Bunia lililoko kwenye jimbo la Ituri nchini humo.

Hatua hiyo inafuatia taarifa ya kwamba kati ya mwezi Januari na tarehe 10 mwezi huu wa Septemba wafungwa 52 walikufa kwa utapiamlo gerezani  humo wakiwemo 7 ambao walikufa kwa njaa. 

Kwa mujibu wa MONUSCO, gereza hilo halijapokea ruzuku yoyote kutoka serikali tangu mwezi Februari mwaka huu. 

Ni kwa mantiki hiyo tarehe 11 mwezi huu wa Septemba, MONUSCO iliandaa mkutano kwa njia ya video na uongozi wa gereza hilo, mawaziri wa afya wa jimbo na haki za binadamu na sheria. 

Baada ya kikao hicho, serikali kuu iliahidi kulipatia jimbo la Ituri fedha zinazotakiwa kwa ajili ya kuhudumia wafungwa, ambapo Camille Zonzi, Mkurugenzi wa gereza la Bunia alishukuru matokeo ya mkutano huo. 

Zonzi amesema, “nafurahi sana kwa sababu nimekuwa nikiahidi kuwa tutashughulikia suala hili. Hata hivyo tatizo bado halijapatiwa suluhu ya kudumu. Gavana Mkuu wa Magereza ametangaza kuwa mishahara na ruzuku ambavyo vilikuwa havijatolewa, vitapatikana Ijumaa au Jumamosi. Lakini hii ni ruzuku tu ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2020. Na sasa hakuna ruzuku na tuko robo ya tatu tayari tuna madeni. Jambo muhimu ni kwamba tupatiwe hizi ruzuku kwa wakati.” 

Uamuzi mwingine uliopitishwa kwenye kikao hicho kilichoratibiwa na MONUSCO ni kurejesha tena shughuli za ushoni, useremala na utengenezaji wa sabuni gerezani humo. 

MONUSCO imesema kuwa hatua hiyo itatoa fursa kwa wafungwa na gereza kujipatia kipato ambacho pia kitatumia kununua chakula kwa ajili ya wafungwa. 

Zonzi amesema kuwa kwa msaada wa wadau ikiwemo MONUSCO, mazao ya shambani yatavunwa haraka na fedha zinazopatikana kupitia kilimo, useremala na utengenezaji sabuni zitatumia pindi ruzuku inapochelewa. 

Audio Credit
Flora Nducha/Assumpta Massoi
Audio Duration
1'47"
Photo Credit
WFP/Jacques David