Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nzige wa jangwani watishia upatikanaji wa chakula Turkana nchini Kenya

Nzige wa jangwani watishia upatikanaji wa chakula Turkana nchini Kenya

Pakua

Nzige vamizi wa jangwani wakiendelea kuharibu mazao kwenye kaunti ya Turkana nchini Kenya, shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO linaendelea na kampeni kubwa ili kupunguza tatizo la ukosefu wa chakula na njia za kujipatia kipato nchini Kenya. Assumpta Massoi na ripoti kamili. 

Lochom Ekiru, mkulima wa Kalemeng’orok akipambana na nzige waliovamia shamba lake la mahindi! Lochom akionekana na huzuni anasema kuwa alitarajia mavuno ili alishe familia yake na kupeleka watoto shuleni, lakini sasa kila kitu kimekwenda. 

Eneo la Kalemng’orok lina ekari 1000 za shamba la kijiji ambako kila kaya hupanda mazao yake ya aina mbalimbali, ziada ikiuzwa sokoni na kiasi kingine kutumiwa na familia lakini mwaka huu kila kitu kimeliwa na nzige wavamizi. Joseph Tirkwel, ni mkulima.“Hawa nzige wavamizi wangalikuja baadaye, angalau ningalikuwa nimevuna mazao yangu kwa ajili ya chakula cha familia. Hii ingalivumilika lakini sasa sijui la kufanya.” 

Wanawake nao walikuwa na bustani yao ya mazao wakipatiwa mafunzo ya upanzi, Anna Akale ni Mwenyekiti wa Bustani hiyo ya Nakukulas. "Tulijifunza jinsi ya kupanda mazao mbalimbali na kuona ni vile ambavyo inasaidia ustawi wa wanawake. Tulikuwa na furaha sana hadi ujio wa nzige ulipokomesha furaha yetu,” 

Upulizaji wa dawa angani na ardhini umefanyika na hata wakulima wenyewe akiwemo Bwana Tirkwel walijaribu kupambana na wadudu hao lakini walishindwa na matumaini yake ni kwa wataalam kutoka FAO ambao amesema ujio wao ni sawa na kwamba Mungu amejibu sala zao na kwamba hawatokata tamaa. 

Mwakilishi wa FAO nchini Kenya Tobias Takavarasha baada ya kauli ya mkulima akafunguka.. “Nilifurahi sana kusikia mkulima akisema kuwa hatokata tamaa. Ninafursahi kuwa FAO na serikali ya kaunti na serikali kuu ya Kenya hatukati tamaa katika kusaidia wakulima kutokomeza wadudu, njaa na magonjwa.” 

Tangu mwezi Januari hadi mapema mwezi huu wa Agosti, zaidi ya ekari 600,000 zimepuliziwa dawa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki ili kutokomeza nzige vamizi wa jangwani.

Audio Credit
Flora Nducha\Assumpta Massoi
Audio Duration
2'13"
Photo Credit
Picha: FAO/G.Tortoli