Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Fit4Five Kenya wapeleka mazoezi ya viungo majumbani wakati huu wa COVID-19

Mradi wa Fit4Five Kenya wapeleka mazoezi ya viungo majumbani wakati huu wa COVID-19

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Kenya linatumia mpango wa michezo kwa maendeleo kusaidia watoto wenye changamoto za kujifunza darasani wakiwemo wale wenye mahitaji maalum ili wasichwe nyuma wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 . 

Mpango huo ulioanza mwaka 2019 hadi sasa umeshasaidia waoto 216 wanaoishi kwenye makazi yasiyo rasmi ya Huruma katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Miongoni mwao ni Buxton Gitimu, mwenye umri wa miaka 11 ambaye mama yake mzazi,  Anne Muthoni anasema kuwa “Buxton alizaliwa mwaka 2009 na alionekana tofauti na watoto wengine. Nilianza kuona ana shida katika kutembea na kuongea, Alipofika wakati wa kwenda shule, Buxton alikuwa haelewi chochote darasani.”

Buxton anapenda kucheza mpira na kuendesha baiskeli hata hivyo kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, hawezi kuendelea na michezo na badala yake wanatakiwa kusalia majumbani.

Buxton aliwakilisha shule ya msingi ya Salama jijini Nairobi, Kenya, kwenye mashinano ya Olimpiki Maalum kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 14 na wenye mahitaij maalum.
UNICEF/Sammy Nyaberi
Buxton aliwakilisha shule ya msingi ya Salama jijini Nairobi, Kenya, kwenye mashinano ya Olimpiki Maalum kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 14 na wenye mahitaij maalum.

UNICEF kwa kutambua umuhimu watoto kama Buxton kuendelea na michezo na mazoezi hata wakati wa COVID-19, imeingia ubia na kamati ya olimpiki maalum ya Kenya, ambapo wanawapatia wanafunzi mpango wa mazoezi.

Vincent Mungai ni meneja wa michezo katika Kamati ya Olimpiki Maalum Kenya na anasema kuwa, “programu ya FIT FOR FIVE inatuwezesha kushirikisha wanamichezo katika mazoezi ya viungo. Tunatuma programu ya mazoezi kwa kupitia simu  za kiganjani za makocha wao, na kisha makocha wanatuma programu hizo kwa wazazi kupitia simu hizo za rununu. Programu imeandaliwa kiasi kwamba ikidhi mahitaji ya watoto wote. Watoto na wazazi wanafanya mazoezi nyumbani.
Baba mzazi wa Buxton, Simon Kabiru anasema kuwa, “hapa nyumbani tunafanya mazoezi kiasi. Kwa kuwa nyumba yetu ni ndogo, tunafanya kile tunachoweza. Mazoezi yamembadilisha sana kwa sababu kuna vitu tunaona anachangamka si kama zamani na hayuko mpweke.”

Buxton anathibitisha kauli ya baba yake akisema kuwa, “nitakapokuwa mtu mzima, nataka kuwa dereva kwa sababu napenda kusafiri. Kufanya mazoezi ni muhimu , inampatia mtu nguvu, afya na unaweza kwenda mbali.”

UNICEF Kenya kupitia mtaalamu wake wa elimu, Rollando Jr Villamero inasema kwamba, “kama ilivyo kwa watoto wengine, watoto wenye ulemavu wanahitaji mazoezi ya viungo ili nao waweze kustawi wakati huu wa janga la COVID-19. Hapa UNICEF Kenya, tunatumia michezo kama mbinu thabiti ya kuendeleza uandikishaji wa watoto shuleni na kuhakikisha wanamaliza masomo. Kupitia mradi huu tumeweza kusaidia watoto wenye ulemavu wa akili kujifunza wakiwa nyumbani na wakati huo huo kuimarisha miili yao.”

Lengo la UNICEF Kenya ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2020, idadi ya wanufaika iwe 500.
 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Flora Nducha
Audio Duration
2'7"
Photo Credit
UNICEF/Sammy Nyaberi