Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi Kaou afaidika na mafunzo ya IFAD kambi ya wakimbizi ya Diffa nchini Niger

Mkimbizi Kaou afaidika na mafunzo ya IFAD kambi ya wakimbizi ya Diffa nchini Niger

Pakua

Mafunzo ya ujasiriliamali kwa vijana wakimbizi yanayotolewa na mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD kwa msaada wa serikali ya Norway na ushirikiano wa serikali ya Niger kwenye kambi ya wakimbizi ya Diffa nchini Niger, yameleta nuru kwa vijana wakimbizi akiweo Ya Kaou aliyekimbia vita vya Boko Haram nchini Nigeria. Jason Nyakundi anaarifu zaidi.

Kwenye kambi ya wakimbizi ya Diffa nchini Niger mkimbizi Ya Kaou mwenye umri wa miaka 24 alikuwa na elimu ndogo sana na bila matarajio yoyote alipowasili kambini hapa baada ya kufurusha na machafuko ya  Boko Haram Kaskazini mwa Nigeria, “hapo kabla tulikuwa tukiishi Nigeria na wazazi wangu, kulikuwa na shambulio la kigaidi hivyo tukakimbias kuja kukaa hapa Diffa.”


Vijana wengi kama Kaou kambini hapo wamekuwa na changamoto kubwa kuanza maisha mapya kwani machafuko katika nchi yao yamewafanya kukatisha masomo na ni vigumu kupata ajira kutokana na elimu ndogo.


Lakini sasa kwa msaada wa IFAD, serikali ya Norway na uongozi wa Diffa wanapatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasiriliamali ambayo yanawawezesha vijana hao akiwemo Kaou kujikimu mafunzo kama kutengeneza sabuni na tambi. Fatchima Keemi ni mmoja wa watoa mafunzo' “tangu walipowasili vijana hawa kumekuwa na mabadiliko, wameweza kuchangamana na wenyeji , kusaidiana na kufanyakazi pamoja, na taratibu wanaanza kusahau madhila waliyokumbana nayo siku za nyuma. Tunawafundisha kwa kutumia bidhaa ambazo zinapatikana na za gharama nafuu ambapo kila mwanamke ambaye amepata mafunzo anaweza kuzipata sokoni na kutengeneza mwenyewe”


Lengo la IFAD ni kuhakikisha vijana hawa wanajitegemea na kuzuka kwa janga la COVID-19 kumefungua mlango mwingine wa kipato chao hasa kwa kuuza sabuni. Na hadi kufikia sasa vijana 80 wameshapatiwa mafunzo akiwemo Kaou, "nahisi nimetulia Diffa na najihisi niko salama nikiwa na marafiki zangu, nina mpango wa kuwa na mustakabali bora hapa Diffa”


Mradi huo una mpango wa kuwafungulia ukurasa mpya wa maisha vijana wengine wengi wakimbizi kama ilivyokuwa kwa Kaou .


 

Audio Credit
Flora Nducha/Jason Nyakundi
Audio Duration
2'13"
Photo Credit
UNICEF/ Cherkaoui