Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkimbizi kutoka Syria awa baraka kwa wenyeji wake Ufaransa

Mkimbizi kutoka Syria awa baraka kwa wenyeji wake Ufaransa

Pakua

Mkimbizi raia wa Syria ambaye hivi sasa anaishi Ufaransa, amejizolea sifa kwa kuandaa chakula kwa ajili ya kuwasambazia wafanyakazi walioko katika mstari wa mbele wa kupambana na janga la COVID-19 katika nchi yake mpya.Hilda Phoya anafafanua zaidi

Nabil Attard mwenye taaluma ya upishi, aliikimbia nchi yake ya Syria na kuingia Ufaransa mwaka 2015 akiwa na familia yake. Mwaka 2018 akafungua mgahawa katika mitaa ya mji wa Orléans akaupa jina Närenj. COVID-19 ilipoanza kusambaa Ufaransa, Nabil akahisi anatakiwa kuchukua hatua. Akaamua kuandaa chakula kwa ajili ya wahudumu wa afya wa kitengo cha magonjwa ya kuambukiza walioko mstari wa mbele katika hospitali ya Orléans na pia kikosi cha zimamoto cha mitaa hiyo akiwapatia chakula cha kisyria, kila wiki.

Nabil anasema,“Wakati wa mzozo nchini Syria, niliona kwa usahihi, ni kwa vipi kunapokuwa na janga au vita katika nchi, mtu anavyopaswa kufanya.”Huku akiendelea kuandaa chakula kwa ajili ya wateja wake na kingine kwa ajili ya wahudu wa afya, Nabil anasema,“Wakati wa shughuli zilipositishwa, tuliwafikiria wale ambao waliendelea kufanya kazi kama vile wauguzi, madaktari, zimamoto, polisi-wale ambao walilazimika kufanya kazi usiku na mchana wakati wa zuio.”

Hapo ndipo aliingiwa na imani ya kutaka kusaidia,“Wakati wa katazo la shughuli za kawaida, nilijihisi natakiwa kuchukua hatua, mara moja, kujitolea kwa wengine na kurudisha kwenye jamii.”Wahudumu katika Hospitali ya Orléans wanaufurahia msaada wa mkimbizi huyu. Mélanie Besse ni mmoja wao anasema,"Lilikuwa jambo la kufurahisha kwa timu yetu kufahamu kuwa watu huko nje wanatufikiria. Tumeamua kwamba mlo ujao tutakaokula kwa pamoja, tutaenda kula katika mgahahawa Närenj.”Kwa pamoja wahudumu wa afya kwa kutumia mikono yao, kila mmoja anaunda alama ya moyo, kuonesha upendo huku wakitabasamu kwa furaha.

Audio Credit
Flora Nducha/Hilda Phoya
Audio Duration
1'56"
Photo Credit
UNICEF/UNI212592/Tremeau