Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yachukua tahadhari kabla ya hatari ya COVID-19 kulinda wakimbizi warohingya

UNHCR yachukua tahadhari kabla ya hatari ya COVID-19 kulinda wakimbizi warohingya

Pakua

Pamoja na kuwa hakuna mgonjwa yeyote wa virusi vya corona, coronavirus">COVID-19 ambaye ameripotiwa miongoni mwa wakimbizi nchini Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linachukua hatua za kujiandaa kukabiliana na mlipuko ikiwemo kujenga wodi za kuwatibu wagonjwa katika maeneo hayo. Taarifa zaidi na John Kibego.
 
(Taarifa ya John Kibego)
 
Ni katika kambi ya wakimbizi ya Kutupalong nchini Bangladesh, wafanyazi wajenzi wako katika harakati za kukimbizana na muda, wengine wanafunga mianzi na wengine wanachanganya mchanga. 
 
Mwakilishi wa UNHCR nchini Bangladesh Steven Corliss anazungumza na maafisa wa UNHCR na pia wafanyakazi wanaofanya kazi katika eneo la ujenzi. Kisha anasema,
 
(Sauti ya Steven Corliss)
 
“mpaka sasa, ni kama tumekuwa na bahati hakuna mgonjwa wa COVID-19 katika makazi ya wakimbizi wa Rohingya kusini mwa Bangladesh lakini tuko katika mbio dhidi ya muda. Tunajaribu kuwa tayari, unaona nyuma yangu kuna kituo cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa ambacho kinaweza kutoa huduma ya haraka kwa watu 150 hadi 200.”
 
Bwana Corliss anasema pia kuwa miundobinu hiyo inajengwa  ili iwahudumie wakimbizi wa Rohingya na jamii wenyeji katika wilaya ya Cox’s Bazar,
 
(Sauti ya Steven Corliss)
 
“vituo kama hivyo vinajengwa katika maeneo tofauti ndani na pia maeneo karibu na makazi ya wakimbizi wa Rohingya. Vituo hivyo vitawahudumia wakimbizi lakini vitawahudumia jamii za wenyeji. Hii ni muhimu, virusi haviangalii hadhi yako, haijalishi kama wewe ni mrohingya au mbangladeshi kwa hivyo kila kitu tunachokifanya, kila hatua zetu lazima ziwe kwa ajili ya jamii zote mbili. Umoja wa Mataifa na wadau wetu mashirika yasiyo ya kiserikali wanafanya kazi kwa ukaribu sana na serikali kuhkikisha kuwa kunakuwa na mipango hiyo.”
 
Serikali ya Bangladeshi, ikiongoza katika mapambano dhidi ya COVID-19, imeweka mpango wa kitaifa ambao unawazingatia wakimbizi. Jumuiya ya misaada ya kibinadamu inaendelea kuhakikisha kuwa wakimbizi wanajumuishwa ipasavyo katika kutekeleza mipango hii na kumefanyika mafunzo ya kukinga ugonjwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na pia uhamasishaji wa utaratibu wa kujisafi.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ John Kibego
Audio Duration
2'10"
Photo Credit
OCHA/Vincent Tremeau