Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa UNDP Mara, Tanzania umezaa matunda

Mradi wa UNDP Mara, Tanzania umezaa matunda

Pakua

Nchini Tanzania mradi wa mafunzo ya kilimo cha kisasa cha nyanya unaofadhiliwa na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP, katika wilaya ya Bunda mkoani Mara umebadili maisha ya wakazi wa eneo hilo na hivyo kufanikisha lengo namba moja la malengo ya maendeleo endelevu, SDGs, la kutokomeza umaskini. Taarifa zaidi na  Flora Nducha.
(Taarifa ya Flora Nducha)
Nats..
Wilaya ya Bunda mkoani Mara tupo katika shamba la kikundi cha wakulima cha Bulamba.
Wakulima hawa wengi wao awali walikuwa wanashughulika na uvuvi lakini sasa wanapata stadi za kilimo cha kisasa cham boga na wanapokea maelekezo kutoka kwa Afisa kilimo Elad Didas Tarimo, hapa  wakitaka kufahamu kuhusu wadudu waharibifu wa nyanya..
Nats…
Ni kutokana na mafunzo hayo kupitia chama cha wakulima wa mboga na matunda Tanzania, TAHA, nyanya zimestawi vizuri na sasa ni heka heka za mavuno,  wanawake,  wanaume na vijana na ndoo zao za nyanya. Hamasa ni kubwa na mchelewaji shambani  hakosi kauli kutoka kwa wenzake…
Nats..
Mkulima huyu ni Tabu Paulo, almaarufu Mama Rock City ni mnufaika wa mradi huu wa mwaka mmoja ambaye anasema.
(Sauti ya Tabu Paulo)
Nimeanza kulima nyanya tarehe 1 mwezi Novemba mwaka 2019. Na kilimo hiki Miongoni mwa changamoto ilikuwa  mvua hapa na pale lakini hizo zote tumezihimili. Nyanya yangu iko sokoni kwa sasa, inang’aa na haina madoa na inavutia. Kwa wanawake wenzangu nawaomba waache kubweteka nyumbani, waje waangalie kilimo tulichofanya hapa kupitia UNDP. Kwa hiyo naomba hii nyanya tukiiuza kwa mauzo tutakayopata kwa mvuno huu wa kwanza tuweze kulima shamba jingine kwa kutumia kilimo cha kisasa zaidi yaani iwe mara mbili ya hapa. Kwa hiyo naomba tuletewe teknolojia zingine mpya za mazao mengine ya bustani ili tuweze kuendeleza mazao mengine mbalimbali ili na sisi tuweze kuajiri watu wengine ili wapitie kwenye mikono ya UNDP na TAHA.
Mradi wa aina hii unaolenga vijana na wanawake unatekelezwa pia katika wilaya za  Same, Arumeru na Busega na UNDP inapanga kupanua zaidi iwapo fedha zitapatikana.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/ Flora Nducha
Audio Duration
2'46"
Photo Credit
UNDP/Sawiche Wamunza