Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uvamizi wa nzige waleta tafrani kwa wakazi nchini Sudan Kusini

Uvamizi wa nzige waleta tafrani kwa wakazi nchini Sudan Kusini

Pakua

Kutokana na uvamizi wa nzige katika maeneo kadhaa ya Afrika kuendelea kuwa tishio kwa uhakika wa chakula na maisha, nchini Sudan Kusini wakulima wameamua kutumia moto na kupiga kelele ili kujaribu kuwazuia nzige huku wakihofia kuwa uvamizi wa nzige hao kuwa wa muda mrefu kwani ni msimu wa kuangua mayai. Jason Nyakundi na taarifa zaidi

(Taarifa ya Jason Nyakundi)

Katika video iliyoandaliwa na shirika la mpango wa chakula duniani, WFP wanaonekana watu wakijaribu kila mbinu ya kupambana na nzige. Wakazi hawa wa Sudan Kusini wameamua kutumia kelele kuwafukuza wadudu hawa waharibifu.

Nzige hawa wa Jangwani waliovamia katika maeneo ya Kenya, Ethiopia, Somalia na hata Sudan Kusini wanatishia mavuno ya miezi miwili kutoka sasa, yaani mwezi wa Mei na Juni na hivyo kuweka hatarini uhakika wa chakula kwa wakulima wadogowadogo wa maeneo haya.

Lotok Joseph Okuera, ni mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa eneo la Magwi Sudan Kusini anasema,

(Sauti ya Okuera)

 “Baadhi ya watu walianza hata kuwaficha watoto wao ndani ya nyumba kwasababu wanafikiri kuwa nzige hawa wanaweza hata kuwala watoto wao.”

Kundi la kwanza la nzige liliingia Sudan Kusini karibu na mpaka wa Uganda mwishoni mwa mwezi Februari wakitafuta eneo zuri la kutaga mayai. Mayai yaliyoanguliwa yameshaonekana kwani huchukua wiki mbili tu kwa mayai kuanguliwa na nzige wadogo hukua na kufikia kuwa nzige wakubwa katika kipindi cha siku 30 au 40.

Thomas Odong, mkulima, anasema,

(Sauti ya Thomas Odong)

 “Nilianza kuwafukuza lakini walikuwa hawaondoki. Walijaa katika eneo hili hata nyuma ya nyumba wapo. Hata katika miembe wapo. Tunaishi kwa mapapai, maembe, parachichi, lakini sasa kama matunda haya yote yataharibiwa na nzige, tutaishi vipi?”

WFP inakadiria kwamba gharama za kukabiliana na madhara ya nzige dhidi ya uhakika wa chakula zinaweza kuwa mara 15 zaidi ya gharama za kuwazuia nzige hao kusambaa hivi sasa.

Matthew Hollingworth, ni Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini anasema,

(Sauti ya Hollingworth)

 “Kwa mara ya kwanza tunaona uwezekano wa amani kuleta mafanikio, na sasa ona kinachotokea! Tunaona uvamizi wa nzige. Kweli mwaka 2020 utakuwa mgumu sana. Tunachokiona Sudan Kusini hii leo ni asilimi 55 ya watu katika janga la uhaba wa chakula hata zaidi. Hakuna nchin nyingine yoyote duniani ambayo watu wengi hivi wanakabiliwa na kiwango hiki cha ukosefu wa chakula.”

Audio Credit
Arnold Kayanda/ Jason Nyakundi
Audio Duration
2'37"
Photo Credit
WFP/Peter Louis